Zaburi 49:13-20
Zaburi 49:13-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao. Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na kifo kitakuwa mchungaji wao; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Miili yao itaoza, kao lao ni kuzimu. Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanipokea. Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapoongezeka. Maana atakapokufa hatachukua chochote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele. Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.
Zaburi 49:13-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe, pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao. Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini, nacho kifo kitawala. Wanyofu watawatawala asubuhi, maumbile yao yataozea kaburini, mbali na majumba yao makubwa ya fahari. Lakini Mungu atakomboa uhai wangu na kaburi, hakika atanichukua kwake. Usitishwe mtu anapotajirika, fahari ya nyumba yake inapoongezeka, kwa maana hatachukua chochote atakapokufa, fahari yake haitashuka pamoja naye. Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri, na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa, atajiunga na kizazi cha baba zake, ambao hawataona kamwe nuru ya uzima. Mwanadamu mwenye utajiri bila ufahamu ni kama wanyama waangamiao.
Zaburi 49:13-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Hayo ndiyo yawapatao wanaojiamini kipumbavu, ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao. Wataongozwa kama kondoo hadi kuzimu, kifo kitakuwa mchungaji wao. Watashuka moja kwa moja kaburini. Miili yao itaozea huko, Kuzimu kutakuwa makao yao. Lakini Mungu ataniokoa na kuzimu. Atanisalimisha kutoka huko. Usihangaike ukiona mtu anatajirika, wala mali yake ikiongezeka zaidi na zaidi. Maana atakapokufa hatachukua chochote, mali yake haitashuka huko chini pamoja naye. Ajapojikuza katika maisha haya, na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa, atajiunga na wazee waliomtangulia kufa, ambao hawawezi kuona tena mwanga. Binadamu hatadumu milele katika fahari yake, atakufa tu kama mnyama.
Zaburi 49:13-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao. Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu. Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha. Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele. Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.