Zaburi 5:1-12
Zaburi 5:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Usikilize maneno yangu, ee Mwenyezi-Mungu, usikie ninavyopiga kite. Usikilize kilio changu, Mfalme wangu na Mungu wangu, maana wewe ndiwe nikuombaye. Ee Mwenyezi-Mungu, alfajiri waisikia sauti yangu, asubuhi nakutolea tambiko yangu, kisha nangojea unijibu. Wewe si Mungu apendaye ubaya; kwako uovu hauwezi kuwako. Wenye majivuno hawastahimili mbele yako; wewe wawachukia wote watendao maovu. Wawaangamiza wote wasemao uongo; wawachukia wauaji na wadanganyifu. Lakini, kwa wingi wa fadhili zako, mimi nitaingia nyumbani mwako; nitakuabudu kuelekea hekalu lako takatifu, nitakusujudia kwa uchaji. Uniongoze, ee Mwenyezi-Mungu, katika uadilifu wako, maana maadui zangu ni wengi; uiweke njia yako wazi mbele yangu. Vinywani mwao hamna ukweli; mioyoni mwao wamejaa maangamizi, wasemacho ni udanganyifu wa kifo, ndimi zao zimejaa hila. Uwaadhibu kwa hatia yao ee Mungu; waanguke kwa njama zao wenyewe; wafukuze nje kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa sababu wamekuasi wewe. Lakini wafurahi wote wanaokimbilia usalama kwako, waimbe kwa shangwe daima. Uwalinde wanaolipenda jina lako, wapate kushangilia kwa sababu yako. Maana wewe Mwenyezi-Mungu wawabariki waadilifu; wawakinga kwa fadhili zako kama kwa ngao.
Zaburi 5:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, uyasikilize maneno yangu, Ukuangalie kutafakari kwangu. Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye. BWANA, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia. Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako; Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao ubatili. Utawaharibu wasemao uongo; BWANA humzira mwuaji na mwenye hila Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu. BWANA, uniongoze kwa haki yako, Kwa sababu yao wanaoniotea. Uisawazishe njia yako mbele ya uso wangu, Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Mtima wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza. Wewe, Mungu, uwapatilize, Na waanguke kwa mashauri yao. Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, Kwa maana wamekuasi Wewe. Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia. Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; BWANA, utamzungushia radhi kama ngao.
Zaburi 5:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee BWANA, tegea sikio maneno yangu, uangalie kupiga kite kwangu. Sikiliza kilio changu ili unisaidie, Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa maana kwako ninaomba. Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee BWANA; asubuhi naleta haja zangu mbele zako, na kusubiri kwa matumaini. Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu mwovu hataishi. Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya. Unawaangamiza wasemao uongo. BWANA huwachukia wamwagao damu na wadanganyifu. Lakini mimi, kwa rehema zako kuu, nitakuja katika nyumba yako, kwa unyenyekevu, nitasujudu kuelekea Hekalu lako takatifu. Niongoze katika haki yako, Ee BWANA, kwa sababu ya adui zangu, nyoosha njia yako mbele yangu. Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo lao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu. Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu! Hila zao ziwe anguko lao wenyewe. Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa kuwa wamekuasi wewe. Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi, waimbe kwa shangwe daima. Ueneze ulinzi wako juu yao, ili wale wapendao jina lako wapate kukushangilia. Kwa hakika, Ee BWANA, unawabariki wenye haki, unawazunguka kwa wema wako kama ngao.
Zaburi 5:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, uyasikilize maneno yangu, Ukuangalie kutafakari kwangu. Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye. BWANA, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia. Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako; Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao uovu. Utawaharibu wasemao uongo; BWANA humchukia mwuaji na mwenye hila Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu. BWANA, uniongoze kwa haki yako, Kwa sababu yao wanaoniotea. Uinyoshe njia yako mbele ya uso wangu, Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Moyo wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza. Wewe, Mungu, uwapatilize, Na waanguke kwa mashauri yao. Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, Kwa maana wamekuasi Wewe. Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga kelele za furaha daima. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia. Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; BWANA, utamzungushia radhi kama ngao.