Zaburi 6:1-10
Zaburi 6:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako; usiniadhibu kwa ghadhabu yako. Unihurumie, ee Mwenyezi-Mungu, nimeishiwa nguvu; uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nataabika mpaka mifupani. Ninahangaika sana rohoni mwangu. Ee Mwenyezi-Mungu, utakawia mpaka lini? Unigeukie, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe; unisalimishe kwa sababu ya fadhili zako. Huko kwa wafu hakuna anayekukumbuka; huko kuzimu ni nani awezaye kukusifu? Niko hoi kwa kilio cha uchungu; kila usiku nalowesha kitanda changu kwa machozi; kwa kulia kwangu naulowesha mto wangu. Macho yangu yamechoka kwa huzuni; yamefifia kwa kutaabishwa na adui. Ondokeni kwangu enyi nyote watenda maovu! Maana Mwenyezi-Mungu amesikia kilio changu. Mwenyezi-Mungu amesikia ombi langu; Mwenyezi-Mungu amekubali sala yangu. Maadui zangu wote wataaibika na kufadhaika; watarudi nyuma na kuaibishwa ghafla.
Zaburi 6:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA, usinikemee kwa hasira yako, Wala usinirudi kwa ghadhabu yako. BWANA, unifadhili, maana ninanyauka; BWANA, uniponye, mifupa yangu imefadhaika. Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, BWANA, hadi lini? BWANA urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru? Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakibubujikia kitanda changu; Nililowesha godoro langu kwa machozi yangu. Macho yangu yameharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi. Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa BWANA ameisikia sauti ya kilio changu. BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu. Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafla wataaibika.
Zaburi 6:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA, usinikemee kwa hasira yako, Wala usinirudi kwa ghadhabu yako. BWANA, unifadhili, maana ninanyauka; BWANA, uniponye, mifupa yangu imefadhaika. Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, BWANA, hata lini? BWANA urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru? Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu. Jicho langu limeharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi. Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa BWANA ameisikia sauti ya kilio changu. BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu. Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.
Zaburi 6:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee BWANA, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. Unirehemu BWANA, kwa maana nimedhoofika; Ee BWANA, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali. Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Mpaka lini, Ee BWANA, mpaka lini? Geuka Ee BWANA, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako. Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa kuzimu? Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha nafurikisha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha viti vyangu vya fahari kwa machozi. Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote. Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana BWANA amesikia kulia kwangu. BWANA amesikia kilio changu kwa huruma, BWANA amekubali sala yangu. Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.