Zaburi 78:40-55
Zaburi 78:40-55 Biblia Habari Njema (BHN)
Mara ngapi walimwasi kule jangwani, na kumchukiza hukohuko nyikani! Walimjaribu Mungu tena na tena, wakamkasirisha huyo Mtakatifu wa Israeli. Hawakuikumbuka nguvu yake, wala siku ile alipowaokoa na maadui zao, alipotenda maajabu nchini Misri, na miujiza kondeni Soani! Aliigeuza ile mito kuwa damu, Wamisri wasipate maji ya kunywa. Aliwapelekea makundi ya nzi waliowasumbua, na vyura waliowatia hasara. Alituma nzige, wakala mavuno yao, na kuharibu mashamba yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, na mitini yao kwa baridi kali. Ngombe wao aliwaua kwa mvua ya mawe, na kondoo wao kwa radi. Aliacha hasira yake kali iwawakie, ghadhabu, chuki na dhiki, na kundi la malaika waangamizi. Aliachilia hasira yake iendelee, wala hakuwaepusha na kifo, bali aliwaangamiza kwa tauni. Aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri; naam, chipukizi wa kwanza kambini mwa Hamu. Kisha aliwahamisha watu wake kama kondoo, akawaongoza jangwani kama kundi la mifugo. Aliwaogoza salama, wala hawakuogopa; lakini bahari iliwafunika maadui zao. Aliwaleta katika nchi yake takatifu, katika mlima aliouteka kwa nguvu yake. Aliyafukuza mataifa mbele yao, akazitoa nchi zao ziwe mali ya Israeli, akayakalisha makabila ya Israeli mahemani mwao.
Zaburi 78:40-55 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakamjaribu Mungu tena na tena; Na kumkasirisha Mtakatifu wa Israeli. Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika uwanda wa Soani. Aligeuza mito yao kuwa damu, Ili wasipate kunywa maji kutoka vijito vyao. Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige matunda ya kazi yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akaifanyia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao kutoka kwa mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Kisha akawaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunika adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kulia. Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha makabila ya Israeli katika hema zao.
Zaburi 78:40-55 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli. Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani. Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa. Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. Akaacha ng’ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume. Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.
Zaburi 78:40-55 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mara ngapi walimwasi jangwani na kumhuzunisha nyikani! Walimjaribu Mungu mara kwa mara, wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. Hawakukumbuka uwezo wake, siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi, siku aliyoonyesha ishara zake za ajabu huko Misri, maajabu yake huko Soani. Aligeuza mito yao kuwa damu, hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao. Aliwapelekea makundi ya mainzi yakawala, na vyura wakawaharibu. Aliruhusu tunutu kuharibu mimea yao, mazao yao kwa nzige. Aliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji. Aliwaachia mifugo yao mvua ya mawe, akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi. Aliwafungulia hasira yake kali, ghadhabu yake, hasira na uadui, na kundi la malaika wa kuharibu. Aliitengenezea njia hasira yake, hakuwaepusha na kifo, bali aliwaachia tauni. Aliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri, matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu. Lakini aliwatoa watu wake kama kundi, akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani. Aliwaongoza salama, wala hawakuogopa, bali bahari iliwameza adui zao. Hivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu, hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa. Aliyafukuza mataifa mbele yao, na kuwagawia nchi zao kama urithi, aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao.