Ufunuo 10:1-7
Ufunuo 10:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi. Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao. Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike. Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni, akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya; isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.
Ufunuo 10:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi kavu, na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo. Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: “Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!” Kisha, yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni, akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, “Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha! Lakini wakati yule malaika wa saba atakapotoa sauti ya tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii.”
Ufunuo 10:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi. Naye akaita kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao. Na ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nilikuwa tayari kuandika. Nami nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie mhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike. Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kulia kuelekea mbinguni, akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na kukawia tena baada ya haya; isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowatangazia watumishi wake hao manabii.
Ufunuo 10:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake ulingʼaa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Mkononi mwake alikuwa ameshika kijitabu kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu. Naye akapiga kelele kwa sauti kuu kama simba anayenguruma. Alipopiga kelele, zile radi saba zikatoa ngurumo zake. Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.” Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni. Naye akaapa kwa Yule aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena! Lakini katika siku zile ambazo huyo malaika wa saba atakapokaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”