Ufunuo 16:1-7
Ufunuo 16:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani.” Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama na wale walioiabudu sanamu yake. Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa. Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu. Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, “Ewe mtakatifu, uliyeko na uliyekuwako! Wewe umetenda sawa kuhukumu mambo hayo. Maana waliimwaga damu ya watu wa Mungu na manabii, nawe umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!” Kisha, nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu Mwenye Nguvu! Hukumu zako ni za kweli na haki!”
Ufunuo 16:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Nendeni mkayamwage yale mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi. Akaenda huyo wa kwanza, akalimimina bakuli lake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake. Na huyo wa pili akalimimina bakuli lake juu ya bahari, ikawa damu, kama damu ya maiti, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa. Na huyo wa tatu akalimimina bakuli lake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu. Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; ndiyo wanayostahili. Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni za kweli, na haki.
Ufunuo 16:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi. Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake. Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa. Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu. Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili. Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.
Ufunuo 16:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.” Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake. Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa. Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu. Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema: “Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa, wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu, kwa sababu umehukumu hivyo; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako na manabii wako, nawe umewapa damu wanywe kama walivyostahili.” Nikasikia madhabahu ikiitikia, “Naam, BWANA Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni kweli na haki.”