Ufunuo 16:8-16
Ufunuo 16:8-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake. Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo. Lakini hawakutubu na kumtukuza Mungu. Kisha, malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakutubu matendo yao mabaya. Kisha, malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ikawekwa kwa ajili ya wafalme kutoka mashariki. Kisha, nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama na kinywani mwa yule nabii wa uongo. Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita ya ile siku kubwa ya Mungu Mwenye Nguvu. “Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko na kuaibika hadharani.” Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.
Ufunuo 16:8-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na huyo wa nne akalimimina bakuli lake juu ya jua, nalo likaruhusiwa kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa na joto kali, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. Na huyo wa tano akalimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. Na huyo wa sita akalimimina bakuli lake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua. Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha lile joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. (Tazama, naja kama mwizi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) Wakawakusanya hadi mahali paitwapo kwa Kiebrania, Harmagedoni.
Ufunuo 16:8-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua. Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni.
Ufunuo 16:8-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto. Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu. Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu, wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu. Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki. Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.” Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedoni kwa Kiebrania.