Ufunuo 17:1-6
Ufunuo 17:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi. Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake.” Kisha, nikakumbwa na Roho mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonesha uzinzi wake. Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo “Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani.” Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno.
Ufunuo 17:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye yale mabakuli saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi; ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wameleweshwa kwa mvinyo ya uasherati wake. Akanichukua katika Roho hadi jangwani, nikaona mwanamke akiwa ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya kukufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi. Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake. Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, Babeli MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI. Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu sana.
Ufunuo 17:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi; ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake. Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi. Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake. Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI. Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu.
Ufunuo 17:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi. Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.” Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake. Kwenye kipaji chake cha uso palikuwa pameandikwa jina: “Siri, Babeli Mkuu, Mama wa makahaba na wa machukizo ya dunia.” Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani, damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Yesu. Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana.