Ufunuo 18:1-8
Ufunuo 18:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng'ao wake. Basi, akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno. Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo.” Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, “Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake. Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimerundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake. Mtendeeni kama alivyowatendea nyinyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Mchanganyieni kikombeni mwake kinywaji kikali maradufu. Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, kulingana na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: ‘Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!’ Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: Ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ana nguvu.”
Ufunuo 18:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake. Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake. Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu. Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe. Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.
Ufunuo 18:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mngʼao wake. Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema: “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu! Umekuwa makao ya mashetani na makazi ya kila pepo mchafu, makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye. Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao, nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.” Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni katikati yake, enyi watu wangu, ili msije mkashiriki dhambi zake, ili msije mkapatwa na pigo lake lolote; kwa kuwa dhambi zake zimelundikana hadi mbinguni, naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake. Mtendee kama yeye alivyotenda; umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda. Katika kikombe chake mchanganyie mara mbili ya kile alichochanganya. Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na utukufu na anasa alizojipatia. Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema, ‘Mimi ninatawala kama malkia; mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’ Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja: mauti, maombolezo na njaa. Naye atateketezwa kwa moto, kwa maana BWANA Mungu amhukumuye ana nguvu.
Ufunuo 18:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya hayo niliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ulio mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake. Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake. Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni mara mbili. Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe. Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.