Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 19:1-10

Ufunuo 19:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; Wokovu na utukufu na nguvu zina Bwana Mungu wetu; kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake. Wakasema mara ya pili, Haleluya. Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne, na wale wenye uhai wanne, wakasujudu na kumwabudu Mungu, aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, Amina, Haleluya. Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Msifuni Mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakuu. Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki. Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu. Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.

Shirikisha
Soma Ufunuo 19

Ufunuo 19:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, “Asifiwe Mungu! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu! Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!” Wakasema, “Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!” Na wale wazee ishirini na wanne, na wale viumbe hai wanne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, “Amina! Asifiwe Mungu!” Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.” Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala! Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari. Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watakatifu). Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu.” Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.”

Shirikisha
Soma Ufunuo 19

Ufunuo 19:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya mikutano mikubwa, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; Wokovu na utukufu na nguvu zina Bwana Mungu wetu; kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake. Wakasema mara ya pili, Haleluya. Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne, na wale wenye uhai wanne, wakasujudu na kumwabudu Mungu, aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, Amina, Haleluya. Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Msifuni Mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakubwa. Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki. Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye ameruhusiwa kuvikwa kitani nzuri, ing'aayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa katika karamu ya arusi ya Mwana-kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu. Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mtumishi mwenzako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.

Shirikisha
Soma Ufunuo 19

Ufunuo 19:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu, kwa maana hukumu zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.” Wakasema tena kwa nguvu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu milele na milele.” Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: “Amen, Haleluya!” Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!” Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Kwa maana BWANA Mungu wetu Mwenyezi anatawala. Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari. Akapewa kitani safi, nyeupe inayongʼaa, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.) Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.” Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”

Shirikisha
Soma Ufunuo 19