Ufunuo 19:10-16
Ufunuo 19:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.” Kisha, nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpandafarasi wake aliitwa “Mwaminifu” na “Kweli”. Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki. Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe. Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni “Neno la Mungu”. Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na yamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi. Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda watu wa mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Nguvu. Juu ya vazi lake, na juu ya paja lake, alikuwa ameandikwa jina: “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”
Ufunuo 19:10-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mtumishi mwenzako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii. Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama muali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. Naye amevikwa vazi lililoloweshwa katika damu, na jina lake anaitwa, Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili kwa upanga huo awapige mataifa. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.
Ufunuo 19:10-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii. Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.
Ufunuo 19:10-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.” Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.” Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili: Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.