Ufunuo 19:17-21
Ufunuo 19:17-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, “Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu. Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapandafarasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: Walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.” Kisha, nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi pamoja na jeshi lake. Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake). Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa madini ya kiberiti. Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao.
Ufunuo 19:17-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njooni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu; mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa. Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake. Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao hao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wakiwa hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti; na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.
Ufunuo 19:17-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu; mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa. Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake. Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti; na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.
Ufunuo 19:17-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, naye akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu, ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo kwa wakubwa.” Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake. Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo aliyekuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.