Ufunuo 20:1-6
Ufunuo 20:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalikamata lile joka – nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani – akalifunga kwa muda wa miaka 1,000. Malaika akalitupa kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka 1,000 itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu. Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa miaka 1,000. (Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka 1,000 itimie). Huu ndio ufufuo wa kwanza. Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka 1,000.
Ufunuo 20:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa na ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia mhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe kwa muda mfupi. Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa mamlaka ya kutoa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala kuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliobakia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.
Ufunuo 20:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.
Ufunuo 20:1-6 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni ibilisi, au Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka elfu. Akamtupa katika lile Shimo, akamfunga humo na kulitia muhuri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa hadi hiyo miaka elfu itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi. Kisha nikaona viti vya utawala vilivyokuwa vimekaliwa na wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Tena nikaona roho za wale waliokatwa vichwa kwa sababu ya ushuhuda wa Isa na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawakuwa wamemsujudu huyo mnyama wala sanamu yake wala hawakupokea ile chapa yake kwenye paji za nyuso zao au kwenye mikono yao. Wakawa hai na kutawala pamoja na Al-Masihi miaka elfu. (Wafu waliosalia hawakufufuka hadi ilipotimia hiyo miaka elfu.) Huu ndio ufufuo wa kwanza. Waliobarikiwa na walio watakatifu ni wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Hao mauti ya pili haina nguvu juu yao, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Al-Masihi, nao watatawala pamoja naye kwa muda wa miaka elfu.