Ufunuo 21:15-21
Ufunuo 21:15-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta zake. Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi, malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: Ulikuwa na urefu, upana na kimo cha kama kilomita 2,400. Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita 60 kwa kipimo cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia. Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani jekundu, la pili johari ya rangi ya samawati, la tatu kalkedoni, la nne zumaridi, la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane zabarajadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasintho, na la kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.
Ufunuo 21:15-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake. Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake ni sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu moja na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa. Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia moja na arubaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, ambacho malaika alitumia. Na ule ukuta ulikuwa umejengwa kwa yaspi, nao mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, kama kioo safi. Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawati; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa tisa yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.
Ufunuo 21:15-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake. Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa. Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika. Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi. Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.
Ufunuo 21:15-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake. Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama kilomita 2,200; urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa. Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144 kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia. Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, ikingʼaa kama kioo. Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi, wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto. Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji huo ilikuwa ya dhahabu safi ingʼaayo kama kioo.