Ufunuo 21:22-27
Ufunuo 21:22-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Nguvu na yule Mwanakondoo ndio hekalu lake. Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo. Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao. Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na usiku humo. Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani. Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.
Ufunuo 21:22-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-kondoo. Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake. Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku. Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake. Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-kondoo.
Ufunuo 21:22-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo. Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake. Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku. Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake. Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.
Ufunuo 21:22-27 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio Hekalu lake. Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake. Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo. Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo. Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.