Ufunuo 9:1-12
Ufunuo 9:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuri kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni. Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi. Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu chochote kilicho kibichi, wala mti wowote, ila wale watu wasio na mhuri wa Mungu katika vipaji vya nyuso zao. Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu. Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia. Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama mataji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu. Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani. Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao. Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki analo jina lake Apolioni. Ole wao, pigo la kwanza limekwisha pita. Tazama, bado yako mapigo mawili, yanakuja baadaye.
Ufunuo 9:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo. Alipolifungua hilo Shimo, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo Shimo. Ndipo katika ule moshi wakatoka nzige wakaenda juu ya nchi, nao wakapewa nguvu kama zile za nge wa duniani. Wakaambiwa wasidhuru nyasi ya nchi, wala mmea wala mti wowote, bali wawadhuru tu wale watu ambao hawana muhuri wa Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Wakaruhusiwa kuwatesa kwa muda wa miezi mitano, lakini wasiwaue. Uchungu wa kuuma kwao ulikuwa kama ule wa mtu aumwapo na nge. Katika siku hizo watu watatafuta kifo lakini hawatakiona, watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia. Wale nzige walikuwa na umbo kama la farasi waliotayarishwa kwa ajili ya vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji za dhahabu na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. Walikuwa na nywele kama za wanawake, na meno yao yalikuwa kama ya simba. Walikuwa na dirii kama za chuma, na sauti za mabawa yao zilikuwa kama ngurumo za farasi wengi na magari mengi yakikimbilia vitani. Walikuwa na mikia yenye miiba ya kuumia kama nge. Nguvu yao ya kutesa watu kwa huo muda wa miezi mitano ilikuwa katika hiyo mikia yao. Walikuwa na mfalme wao, ambaye ni malaika wa lile Shimo, ambaye jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani ni Apolioni. Ole ya kwanza imepita, bado nyingine mbili zinakuja.
Ufunuo 9:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la kuzimu, kukatoka moshi wa tanuri kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa kuzimu. Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani, wakapewa nguvu kama ya nge. Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso. Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na nge. Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia. Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani. Walikuwa na mikia na miiba kama nge, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani Mwangamizi. Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.
Ufunuo 9:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni. Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi. Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wo wote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao. Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu. Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia. Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu. Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani. Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao. Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni. Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili, zinakuja baadaye.