Waroma 13:8-14
Waroma 13:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza sheria. Maana, amri hizi: “Usizini; Usiue; Usitamani;” na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, upendo ni utimilifu wa sheria. Zaidi ya hayo, nyinyi mnajua tumo katika wakati gani: Sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu uko karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini. Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu. Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha.
Waroma 13:8-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria. Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu uko karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.
Waroma 13:8-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria. Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.
Waroma 13:8-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria. Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa sheria. Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia kuliko hapo kwanza tulipoamini. Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru. Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali jivikeni Bwana Isa Al-Masihi, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.