Waroma 3:1-8
Waroma 3:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kila usemapo, maneno yako ni ya kweli; na katika hukumu, wewe hushinda.” Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu? Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili!
Waroma 3:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Myahudi ana nini zaidi? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu. Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutoamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? La hasha! Mungu aonekane kuwa kweli japo kila mtu ni mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulikane kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu. Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.) Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu? Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi? Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki.
Waroma 3:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu. Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu. Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.) Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu? Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi? Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki.
Waroma 3:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara? Kuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa lile Neno halisi la Mungu. Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu? La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa: “Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena, na ukashinde utoapo hukumu.” Ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.) La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angehukumuje ulimwengu? Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonyesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?” Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja?” Wao wanastahili hukumu yao.