Waroma 3:21-26
Waroma 3:21-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.
Waroma 3:21-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na Torati na Manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aoneshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.
Waroma 3:21-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.
Waroma 3:21-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.