Zekaria 10:1-3
Zekaria 10:1-3 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwombeni Mwenyezi-Mungu awape mvua za masika. Mwenyezi-Mungu ndiye aletaye mawingu ya mvua; ndiye awapaye watu mvua za rasharasha, na kustawisha mimea shambani kwa ajili ya wote. Vinyago vyao vya kupigia ramli ni upuuzi mtupu, na waaguzi wao wanaagua uongo; watabiri wao wanatabiri ndoto za danganyifu, na kuwapa watu faraja tupu. Ndio maana watu wa Yuda wanatangatanga kama kondoo; wanataabika kwa kuwa wamekosa mchungaji. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nimewaka hasira dhidi ya hao wachungaji, nami nitawaadhibu hao viongozi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nitalitunza kundi langu, ukoo wa Yuda. Nitawafanya kuwa farasi wangu hodari wa vita.
Zekaria 10:1-3 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA aletaye mawingu ya mvua, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi shambani. Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo watu wanatangatanga kama kondoo, wanateseka kwa kukosa mchungaji. Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.
Zekaria 10:1-3 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni. Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji. Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.
Zekaria 10:1-3 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwombeni BWANA mvua wakati wa vuli; ndiye BWANA atengenezaye mawingu ya tufani. Huwapa watu manyunyu ya mvua, pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu. Sanamu huzungumza udanganyifu, waaguzi huona maono ya uongo; husimulia ndoto ambazo si za kweli, wanatoa faraja batili. Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo walioonewa kwa kukosa mchungaji. “Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa kuwa BWANA Mwenye Nguvu Zote atalichunga kundi lake, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi mwenye kiburi akiwa vitani.