Zekaria 2:2-13
Zekaria 2:2-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo nikasema, Unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake ulivyo na urefu wake ulivyo. Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu, na malaika mwingine akatoka ili kuonana naye; naye akamwambia, Piga mbio, kamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa na watu, kama vijiji visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake. Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake. Haya! Haya! Ikimbieni nchi ya kaskazini, asema BWANA; kwa maana mimi nimewatawanya ninyi kama pepo nne za mbinguni, asema BWANA. Haya! Ee Sayuni, jiponye, wewe ukaaye pamoja na binti Babeli. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake. Kwa maana, tazama, nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia; nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma. Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema BWANA. Na mataifa mengi watajiunga na BWANA katika siku ile, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yako, nawe utajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwako. Na BWANA atairithi Yuda, iwe sehemu yake katika nchi takatifu, naye atachagua Yerusalemu tena. Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za BWANA; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu.
Zekaria 2:2-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nikamuuliza, “Unakwenda wapi?” Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.” Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo. Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema BWANA, ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’ “Njooni! Njooni! Kimbieni mtoke katika nchi ya kaskazini,” asema BWANA, “Kwa kuwa nimewatawanya kwenye pande nne za mbingu,” asema BWANA. “Njoo, ee Sayuni! Kimbia, wewe ukaaye ndani ya Binti Babeli!” Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Baada ya yeye kuniheshimu na kunituma mimi dhidi ya mataifa yaliyokuteka nyara, kwa kuwa yeyote awagusaye ninyi, anaigusa mboni ya jicho lake, hakika nitauinua mkono wangu dhidi yao ili watumwa wao wawateke nyara. Ndipo mtakapojua ya kwamba BWANA Mwenye Nguvu Zote amenituma. “Piga kelele na ufurahie, ee Binti Sayuni, kwa maana ninakuja, nami nitaishi miongoni mwenu,” asema BWANA. “Mataifa mengi yataunganishwa na BWANA siku hiyo, nao watakuwa watu wangu. Nitaishi miongoni mwenu nanyi mtajua kwamba BWANA Mwenye Nguvu Zote amenituma kwenu. BWANA atairithi Yuda kama fungu lake katika nchi takatifu na atachagua tena Yerusalemu. Tulieni mbele za BWANA, enyi watu wote, kwa sababu ameinuka kutoka makao yake matakatifu.”
Zekaria 2:2-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nikamwuliza, “Unakwenda wapi?” Naye akanijibu, “Ninakwenda kuupima urefu na upana wa mji wa Yerusalemu.” Yule malaika aliyezungumza nami akawa anamwendea malaika mwingine ambaye alikuwa anamjia. Basi, huyo malaika aliyezungumza nami akamwambia huyo mwenzake, “Kimbia ukamwambie yule kijana kwamba si lazima mji wa Yerusalemu uwe na kuta, la sivyo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha wakazi wake wengi na mifugo itakayokuwa ndani yake. Mwenyezi-Mungu asema kuwa yeye mwenyewe atakuwa ukuta wa moto kuulinda mji huo pande zote, naye atakaa humo kwa utukufu wake.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Haya! Kimbieni kutoka nchi ya kaskazini ambako mimi nilikuwa nimewatawanya kila upande. Haraka! Nyinyi nyote mnaokaa katika nchi ya Babuloni, kimbilieni huko mjini Siyoni!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ambaye kwa utukufu wake amenituma, asema hivi juu ya mataifa yaliyowateka nyara watu wake: “Hakika, anayewagusa nyinyi anagusa mboni ya jicho langu. Naam, nitachukua hatua dhidi ya hao waliowatekeni nyara, nao watatekwa nyara na wale waliowafanya watumwa wao.” Hapo ndipo mtakapojua kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndiye aliyenituma. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Siyoni, imbeni na kufurahi kwa kuwa ninakuja na kukaa kati yenu. Mataifa mengi yatajiunga nami Mwenyezi-Mungu, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yenu.” Mambo hayo yatakapotukia ndipo mtakapojua kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndiye aliyenituma kwenu. Watu wa Yuda watakuwa tena mali ya pekee ya Mwenyezi-Mungu katika nchi takatifu, na mji wa Yerusalemu utakuwa tena mji wake aliouchagua. Enyi wanadamu wote, nyamazeni mbele ya Mwenyezi-Mungu, maana, yeye anakuja kutoka makao yake matakatifu.
Zekaria 2:2-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo nikasema, Unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake ulivyo na urefu wake ulivyo. Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu, na malaika mwingine akatoka ili kuonana naye; naye akamwambia, Nenda mbio ukamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa na watu, kama vijiji visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake. Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake. Haya! Haya! Ikimbieni nchi ya kaskazini, asema BWANA; kwa maana mimi nimewatawanya ninyi kama pepo nne za mbinguni, asema BWANA. Haya! Ee Sayuni, jiponye, wewe ukaaye pamoja na binti Babeli. Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake. Kwa maana, tazama, nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia; nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma. Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema BWANA. Na mataifa mengi watajiunga na BWANA katika siku ile, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yako, nawe utajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwako. Na BWANA atairithi Yuda, iwe sehemu yake katika nchi takatifu, naye atachagua Yerusalemu tena. Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za BWANA; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu.