Zekaria 3:6-10
Zekaria 3:6-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha malaika wa BWANA akamshuhudia Yoshua, akisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu. Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako waketio mbele yako; maana hao ni watu walio ishara; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi. Maana, litazame jiwe hili nililoliweka mbele ya Yoshua; katika jiwe moja yako macho saba; tazama, nitachora machoro yake, asema BWANA wa majeshi, nami nitauondoa uovu wa nchi ile katika siku moja. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ninyi mtamwalika kila mtu jirani yake chini ya mzabibu, na chini ya mtini.
Zekaria 3:6-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwonya kuhani mkuu Yoshua, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Ukifuata mwongozo wangu na kuyazingatia maagizo niliyokupa, basi, utaisimamia nyumba yangu na nyua zake. Nami nitakuwezesha kuingia katika utumishi wangu kama hawa wanaosimama mbele yangu. Sasa sikiliza kwa makini, ewe Yoshua, kuhani mkuu; sikilizeni pia enyi makuhani wenzake mlio pamoja naye, nyinyi mlio ishara ya wakati mzuri ujao: Nitamleta mtumishi wangu aitwaye Tawi. Kumbukeni kuwa nimeweka mbele ya Yoshua jiwe moja lenye nyuso saba. Nami nitachora maandishi juu yake, na kwa siku moja tu, nitaiondoa dhambi ya nchi hii. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Siku hiyo, kila mmoja wenu atamwalika mwenzake kufurahia amani na utulivu katika shamba lake la mizabibu na la mitini.’”
Zekaria 3:6-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha malaika wa BWANA akamshuhudia Yoshua, akisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Ikiwa utaenda katika njia zangu, na kushika maagizo yangu, basi utaihukumu nyumba yangu, na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa haki ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu. Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako wanaoketi mbele yako; maana hao ni watu walio ishara ya mambo yajayo; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi. Maana, litazame jiwe hili nililoliweka mbele ya Yoshua; katika jiwe moja ziko nyuso saba; tazama, nitachonga maandishi yake, asema BWANA wa majeshi, nami nitauondoa uovu wa nchi hii katika siku moja. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ninyi mtamwalika kila mtu jirani yake chini ya mzabibu, na chini ya mtini.
Zekaria 3:6-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malaika wa BWANA akamwamuru Yoshua: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Ikiwa utakwenda katika njia zangu na kushika masharti yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuwa na amri juu ya nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa. “ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninakwenda kumleta mtumishi wangu, Tawi. Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja. “ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.”