Zekaria 5:1-4
Zekaria 5:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilipotazama tena niliona kitabu kinaruka angani. Yule malaika akaniuliza, “Unaona nini?” Nami nikamjibu, “Ninaona kitabu kinaruka angani; urefu wake ni mita tisa na upana wake ni mita nne na nusu.” Basi, yeye akaniambia, “Ndani ya kitabu hicho kumeandikwa laana ambayo itaikumba nchi nzima. Upande mmoja imeandikwa kwamba wezi wote watafukuzwa nchini, na upande mwingine imeandikwa kwamba wote wenye kuapa uongo kadhalika watafanyiwa vivyo hivyo. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema kuwa yeye mwenyewe ataipeleka laana hiyo. Itapenya kila nyumba ya mwizi na kila nyumba ya mwenye kuapa uongo kwa kutumia jina lake; itakaa humo na kuteketeza nyumba hiyo yote, mbao na mawe.”
Zekaria 5:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la kitabu lirukalo. Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la kitabu lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atakatiwa mbali kama ilivyoandikwa upande, na kwa hiyo kila aapaye kwa uongo atakatiliwa mbali kama ilivyo andikwa upande wa pili. Nitaituma itokee, asema BWANA wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi, na katika nyumba ya yeyote aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katika nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.
Zekaria 5:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la chuo lirukalo. Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la chuo lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili. Nitaituma itokee, asema BWANA wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.
Zekaria 5:1-4 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kilichoruka! Akaniuliza, “Unaona nini?” Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka chenye, urefu wa dhiraa ishirini na upana wa dhiraa kumi.” Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali. BWANA Mwenye Nguvu Zote asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ”