Zekaria 7:1-10
Zekaria 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Dario, siku ya nne ya mwezi wa tisa, yaani Kislevu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi Zekaria. Watu wa mji wa Betheli walikuwa wamewatuma Sharesa na Regem-meleki pamoja na watu wao kumwomba Mwenyezi-Mungu fadhili zake, na kuwauliza makuhani wa hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi na manabii swali hili: “Je, tuendelee kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano kama tulivyofanya kwa muda wa miaka mingi sasa?” Hapo, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi likanijia: “Waambie wakazi wote wa nchi na makuhani hivi: ‘Kwa muda wa miaka sabini iliyopita, nyinyi mmekuwa mkifunga na kuomboleza mnamo mwezi wa tano na wa saba. Je, mnadhani mlifunga kwa ajili yangu? Je, mnapokula na kunywa, si mnakula na kunywa kwa ajili yenu wenyewe?’ Haya ndiyo mambo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu niliwaambieni kupitia kwa manabii wa hapo kwanza, wakati mji wa Yerusalemu ulikuwa umestawi na wenye wakazi tele, na wakati ambapo kulikuwa na wakazi wengi katika miji ya kandokando yake na katika eneo la Negebu na nyanda za Shefela.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mimi Zekaria: “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Amueni kwa haki, muwe na upole na huruma nyinyi kwa nyinyi. Msiwadhulumu wajane, yatima, wageni au maskini; msikusudie mabaya mioyoni mwenu dhidi yenu wenyewe.
Zekaria 7:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, siku ya nne ya mwezi wa tisa, yaani, Kislevu. Basi watu wa Betheli walikuwa wamewatuma Shareza na Regem-meleki, na watu wao, ili kuomba fadhili za BWANA, na kusema na makuhani wa nyumba ya BWANA wa majeshi, na hao manabii, ya kwamba, Je! Yanipasa kulia katika mwezi wa tano, na kufunga, kama nilivyofanya miaka hii mingi iliyopita? Ndipo neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema, Waambie watu wote wa nchi, na hao makuhani, ukisema, Hapo mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na mwezi wa saba, katika miaka hiyo sabini, je, Mlifunga kwa ajili yangu? Na wakati mnapokula chakula na kunywa, je, Hamli kwa ajili ya nafsi zenu, na kunywa kwa ajili ya nafsi zenu? Je, Hayo siyo maneno aliyoyasema BWANA kwa vinywa vya manabii wa zamani, wakati Yerusalemu ulipokaliwa na watu na kufanikiwa, na miji yake iliyokuwa ikiuzunguka; na wakati ule ambao nchi ya Negebu na Shefela ilipokuwa ikikaliwa na watu? Kisha neno la BWANA likamjia Zekaria, kusema, BWANA wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.
Zekaria 7:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, siku ya nne ya mwezi wa kenda, yaani, Kisleu. Basi watu wa Betheli walikuwa wamewatuma Shareza na Regem-meleki, na watu wao, ili kuomba fadhili za BWANA, na kusema na makuhani wa nyumba ya BWANA wa majeshi, na hao manabii, ya kwamba, Je! Yanipasa kulia katika mwezi wa tano, na kujitenga na watu, kama nilivyofanya miaka hii mingi iliyopita? Ndipo neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema, Waambie watu wote wa nchi, na hao makuhani, ukisema, Hapo mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na mwezi wa saba, katika miaka hiyo sabini, je! Mlinifungia mimi kwa lo lote; mlinifungia mimi? Na wakati mlapo chakula na kunywa, je! Hamli kwa ajili ya nafsi zenu, na kunywa kwa ajili ya nafsi zenu? Je! Hayo siyo maneno aliyoyasema BWANA kwa vinywa vya manabii wa zamani, wakati Yerusalemu ulipokaliwa na watu na kufanikiwa, na miji yake iliyokuwa ikiuzunguka; na wakati ule ambao nchi ya Negebu na Shefela ilipokuwa ikikaliwa na watu? Kisha neno la BWANA likamjia Zekaria, kusema, BWANA wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.
Zekaria 7:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa nne wa utawala wa Mfalme Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria siku ya nne ya mwezi wa tisa, mwezi wa Kisleu. Watu wa Betheli walikuwa wamemtuma Shareza na Regem-Meleki pamoja na watu wao, kumsihi BWANA kwa kuwauliza makuhani wa nyumba ya BWANA Mwenye Nguvu Zote na manabii, “Je, imempasa kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi?” Kisha neno la BWANA Mwenye Nguvu Zote likanijia kusema: “Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu? Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu? Je, haya sio maneno ya BWANA aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefala zikiwa zimekaliwa na watu?’ ” Neno la BWANA likamjia tena Zekaria: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’