Zekaria 9:9-13
Zekaria 9:9-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwanapunda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiria mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia. Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Rudini katika ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu. Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawachochea wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Ugiriki, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.
Zekaria 9:9-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia. Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu. Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.
Zekaria 9:9-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Shangilieni sana enyi watu wa Siyoni! Paazeni sauti, enyi watu wa Yerusalemu! Tazama, mfalme wenu anawajieni, anakuja kwa shangwe na ushindi! Ni mpole, amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda. Atatokomeza magari ya vita nchini Efraimu, na farasi wa vita kutoka mjini Yerusalemu; pinde za vita zitavunjiliwa mbali. Naye ataleta amani miongoni mwa mataifa; utawala wake utaenea toka bahari hata bahari, toka mto Eufrate hata miisho ya dunia. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwa sababu ya agano langu nanyi, agano lililothibitishwa kwa damu, nitawakomboa wafungwa wenu walio kama wamefungwa katika shimo tupu. Enyi wafungwa wenye tumaini; rudini kwenye ngome yenu. Sasa mimi ninawatangazieni: Nitawarudishieni mema maradufu. Yuda nitamtumia kama uta wangu; Efraimu nimemfanya mshale wangu. Ee Siyoni! Watu wako nitawatumia kama upanga kuwashambulia watu wa Ugiriki; watakuwa kama upanga wa shujaa.”
Zekaria 9:9-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Shangilia sana, ee Binti Sayuni! Piga kelele, Binti Yerusalemu! Tazama, Mfalme wako anakuja kwako, ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mpole, naye amepanda punda, mwana-punda, mtoto wa punda. Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu na farasi wa vita kutoka Yerusalemu, nao upinde wa vita utavunjwa. Atatangaza amani kwa mataifa. Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari, na kutoka Mto Frati hadi mwisho wa dunia. Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya Agano langu nawe, nitawaacha huru wafungwa wako watoke kwenye shimo lisilo na maji. Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata sasa ninatangaza kwamba nitawarejesheeni maradufu. Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu, nitamfanya Efraimu mshale wangu. Nitawainua wana wako, ee Sayuni, dhidi ya wana wako, ee Uyunani, na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.