Yohana 14:1-11
Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.
Yn 14:1-11