Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi yu juu yangu,
kwa sababu Mwenyezi Mungu amenipaka mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwafariji waliovunjika moyo,
kuwatangazia mateka uhuru wao,
na hao waliofungwa
habari za kufunguliwa kwao;
kutangaza mwaka wa Mwenyezi Mungu uliokubaliwa,
na siku ya kisasi ya Mungu wetu,
kuwafariji wote wanaoomboleza,
na kuwapa mahitaji
wale wanaohuzunika katika Sayuni,
ili kuwapa taji za uzuri badala ya majivu,
mafuta ya furaha badala ya maombolezo,
vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.
Nao wataitwa mialoni ya haki,
pando la Mwenyezi Mungu,
ili kuonesha utukufu wake.