1 Wakorintho 16
16
Changizo kwa ajili ya watakatifu
1Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makundi ya waumini ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake, na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4Ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
Mahitaji binafsi
5Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. 6Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. 7Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana Isa akipenda. 8Lakini nitakaa Efeso hadi wakati wa Pentekoste, 9kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
10Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana Isa, kama mimi nifanyavyo. 11Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.
12Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.
Maneno ya mwisho
13Kesheni; simameni imara katika imani; kuweni mashujaa na hodari. 14Fanyeni kila kitu katika upendo.
15Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio walikuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, 16mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. 17Nilifurahi Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. 18Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.
Salamu za mwisho
19Makundi ya waumini wa jimbo la Asia wanawasalimu.
Akila na Prisila#16:19 kwa Kiyunani ni Priska pamoja na kundi la waumini walioko nyumbani mwao wanawasalimu sana katika Bwana Isa.
20Ndugu wote walio hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
21Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.
22Kama mtu yeyote hampendi Bwana Isa Al-Masihi, na alaaniwe. Bwana wetu Isa, njoo#16:22 kwa Kiaramu ni Marana tha.
23Neema ya Bwana Isa iwe nanyi.
24Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Al-Masihi Isa. Amen.
Currently Selected:
1 Wakorintho 16: NENO
Highlight
Share
Copy

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.