2 Timotheo 3
3
Hatari za siku za mwisho
1Lakini yakupasa ufahamu jambo hili: kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. 2Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, 3wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, 4wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wanaopenda anasa kuliko kumpenda Mungu: 5wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu kama hao.
6Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. 7Hawa hujifunza siku zote, lakini kamwe hawawezi kuufikia ujuzi wa kweli. 8Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo watu hawa hupingana na kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. 9Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile upumbavu wa hao watu wawili ulivyokuwa dhahiri.
Paulo amwagiza Timotheo
10Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, 11mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana Isa aliniokoa katika hayo yote. 12Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Al-Masihi Isa atateswa. 13Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. 14Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15na jinsi tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kupitia kwa imani katika Al-Masihi Isa. 16Maandiko yote yamevuviwa na Mungu, na yafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
Currently Selected:
2 Timotheo 3: NENO
Highlight
Share
Copy
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fen.png&w=128&q=75)
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.