Mwanzo 39
39
Yosefu Na Mke Wa Potifa
1 Wakati huu Yosefu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yosefu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.
2 Bwana alikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. 3 Potifa alipoona kuwa Bwana alikuwa pamoja na Yosefu na kwamba Bwana alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4 Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. 5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, Bwana aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yosefu. Baraka ya Bwana ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.
Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia; 7baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yosefu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”
8 Lakini Yosefu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu chochote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi. 9 Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” 10Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, Yosefu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.
11 Siku moja Yosefu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba. 12 Mke wa Potifa akashika vazi Yosefu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yosefu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.
13Yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba, 14 akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele. 15Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.”
16Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani. 17 Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki. 18Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.”
19Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka. 20 Potifa akamchukua Yosefu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa.
Lakini wakati Yosefu alipokuwa huko gerezani, 21 Bwana alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. 22Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. 23 Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yosefu, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja na Yosefu akimfanikisha kwa kila alichofanya.
Currently Selected:
Mwanzo 39: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.