YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 58

58
Mfungo Wa Kweli
1 “Piga kelele, usizuie.
Paza sauti yako kama tarumbeta.
Watangazieni watu wangu uasi wao,
na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.
2 Kwa maana kila siku hunitafuta,
wanaonekana kutaka kujua njia zangu,
kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa,
na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake.
Hutaka kwangu maamuzi ya haki,
nao hutamani Mungu awakaribie.
3 Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?
Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’
“Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka
na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.
4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,
na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.
Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo
na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.
5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,
siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?
Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,
na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu?
Je, huo ndio mnaouita mfungo,
siku iliyokubalika kwa Bwana?
6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:
kufungua minyororo ya udhalimu,
na kufungua kamba za nira,
kuwaweka huru walioonewa,
na kuvunja kila nira?
7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa
na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,
unapomwona aliye uchi, umvike,
wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?
8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko
na uponyaji wako utatokea upesi;
ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,
na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.
9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,
utalia kuomba msaada,
naye atasema: Mimi hapa.
“Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,
na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,
10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu
na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,
ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,
nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.
11 Bwana atakuongoza siku zote,
atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,
naye ataitia nguvu mifupa yako.
Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,
kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.
12Watu wako watajenga tena magofu ya zamani
na kuinua misingi ya kale;
utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka,
Mwenye Kurejeza Barabara za Makao.
13 “Kama ukitunza miguu yako isivunje Sabato,
na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu,
kama ukiita Sabato siku ya furaha
na siku takatifu ya Bwana ya kuheshimiwa,
kama utaiheshimu kwa kutoenenda
katika njia zako mwenyewe,
na kutokufanya yakupendezayo
au kusema maneno ya upuzi,
14 ndipo utakapojipatia furaha yako katika Bwana,
nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi
na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.”
Kinywa cha Bwana kimenena haya.

Currently Selected:

Isaya 58: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in