Yeremia 40
40
Yeremia Aachiwa Huru
1 Neno likamjia Yeremia kutoka kwa Bwana baada ya Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli. 2 Kiongozi wa walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “Bwana Mungu wako aliamuru maafa haya kwa mahali hapa. 3 Sasa Bwana ameyaleta haya, amefanya sawasawa na vile alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya Bwana na hamkumtii. 4 Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Twende pamoja mpaka Babeli ikiwa unataka, nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.” 5 Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.”
Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake. 6 Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.
Gedalia Auawa
(2 Wafalme 25:22-26)
7 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli, 8 wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 9 Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu. 10 Mimi mwenyewe nitakaa Mispa ili kuwawakilisha mbele ya Wakaldayo wanaotujia, lakini ninyi mtavuna divai, matunda ya kiangazi na mafuta, nanyi mtaweka katika vyombo vyenu vya kuhifadhia, na kuishi katika miji mliyojitwalia.”
11 Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, Edomu na nchi nyingine zote waliposikia kwamba mfalme wa Babeli ameacha mabaki ya watu katika Yuda na amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kuwa mtawala wao, 12 wakarudi wote katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mispa, kutoka nchi zote ambazo walikuwa wametawanywa. Nao wakavuna divai na matunda tele wakati wa kiangazi.
13Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi wakamjia Gedalia huko Mispa 14 na kumwambia, “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini.
15 Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia Gedalia kwa siri huko Mispa, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, wala hakuna atakayejua. Kwa nini akuue na kusababisha Wayahudi wote waliokuzunguka watawanyike, na mabaki wa Yuda waangamie?”
16 Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo kama hilo! Unalosema kuhusu Ishmaeli si kweli.”
Currently Selected:
Yeremia 40: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.