Ayubu Utangulizi
Utangulizi
Kitabu cha Ayubu kimepewa jina la mhusika mkuu ambaye ni mtu mwenye haki mbele za Mungu na aliyekuwa tajiri sana. Ayubu maana yake ni “Yule anayemrudia Mungu daima.” Hata baada ya kuondokewa na vitu vyote alivyokuwa navyo na kuteseka kwa majipu hatari, Ayubu bado alikiri kumpenda Mungu. Lakini marafiki wa Ayubu walisisitiza kwamba alikuwa anateseka kwa sababu alikuwa ametenda dhambi, na kwamba hiyo ilikuwa ni adhabu yake. Ayubu alijitetea kwa kusisitiza kwamba hajafanya uovu ambao ungemsabibishia hiyo adhabu na ya kwamba yeye anamwamini Mungu. Ndipo Mungu alipozungumza na kuonyesha uwezo wake mkubwa. Mwisho wa yote Ayubu alikubali kwamba Mungu ni mkuu na wa ajabu kwetu, kiasi kwamba hatuwezi kumwelewa.
Mwandishi
Haijulikani kwa dhahiri ni nani aliyekiandika kitabu hiki, huenda ikawa ni Ayubu. Wengine hudhani ni Mose, Solomoni au Elihu.
Kusudi
Kitabu hiki kinaonyesha uweza na uaminifu wa Mungu, na pia kinathibitisha maana ya imani ya kweli ya mtu wa Mungu. Kitabu hiki kinaonyesha baraka zinazoandamana na ushindi baada ya majaribu. Kwa hiyo kazi ya majaribu ambayo Mungu anayaruhusu ni kutudhibitisha katika imani. Kitabu hiki kinazungumzia swali hili: “Ni kwa nini wenye haki huteseka?”
Mahali
Kuna uwezekano kwamba nchi ya Usi ilikuwa kaskazini mashariki mwa Palestina, karibu na jangwa iliyo katikati ya Dameski na Mto Frati.
Tarehe
Tarehe ya kuandikwa kwa kitabu hiki haijulikani; kinadhaniwa kuwa kitabu cha zamani sana, huenda kuliko vingine vyote katika Biblia. Yawezekana kuwa mambo yalioandikwa kwenye kitabu hiki yalitendeka kati ya 2000–1800 K.K.
Wahusika Wakuu
Ayubu, Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, Sofari Mnaamathi, na Elihu wa kabila la Buzi.
Wazo Kuu
Mungu ametuwekea ugo pande zote. Hivyo Shetani hawezi kutushambulia bila Mungu kujua, lakini wakati mwingine Mungu hutoa ruhusa ili kumthibitishia adui juu ya uelekevu na uadilifu wa mtu wake. Hivyo basi, kumtumaini Mungu wakati wote na katika hali zote huleta ushindi dhidi ya Shetani.
Mambo Muhimu
Kujaribiwa kwa Ayubu, mazungumzo na rafiki zake, na vile Mungu alimnenea na kumbariki baadaye na watoto na mali nyingi kushinda hapo mwanzo.
Mgawanyo
Habari za awali, na Ayubu kujaribiwa (1:1–2:13)
Mazungumzo ya Ayubu na rafiki zake watatu (3:1–31:40)
1. Mungu anahusikaje na mateso ya Ayubu? (3:1–14:22)
2. Je, watu waovu huwa wanateseka mara zote? (15:1–21:34)
3. Je, Ayubu ana hatia ya kuwa na dhambi ya siri? (22:1–31:40)
Elihu anamjibu Ayubu na kuwakemea marafiki zake (32:1–37:24)
Mungu anamjibu Ayubu (38:1–41:34)
Mwisho (42:1-17).
Currently Selected:
Ayubu Utangulizi: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.