YouVersion Logo
Search Icon

Marko 1

1
Huduma ya Yahya
(Marko 1:1-13)
Yahya atayarisha njia
(Mathayo 3:1-12; Luka 3:1-8; Yohana 1:19-28)
1Mwanzo wa Injili ya Isa Al-Masihi, Mwana wa Mungu#1:1 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili., 2kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:
“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako”#1:2 Malaki 3:1:
3“sauti ya mtu aliaye nyikani,
‘Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu,
yanyoosheni mapito yake.’#1:3 Isaya 40:3
4Yahya alikuja akibatiza#1:4 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5Watu kutoka Yudea yote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. 6Yahya alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Alikula nzige na asali ya mwitu. 7Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. 8Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho wa Mungu.”
Isa abatizwa
(Mathayo 3:13-17; Luka 3:21-22)
9Wakati huo Isa akaja kutoka Nasiri ya Galilaya, naye akabatizwa na Yahya katika Mto Yordani. 10Isa alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho wa Mungu akishuka juu yake kama hua. 11Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
Isa ajaribiwa nyikani
(Mathayo 4:1-11; Luka 4:1-13)
12Wakati huo huo, Roho wa Mungu akamwongoza Isa hadi nyikani, 13naye Isa akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama pori, nao malaika wakamhudumia.
Huduma ya Isa huko Galilaya
(Marko 1:14–9:50)
Isa aanza kuhubiri
(Mathayo 4:12-17; Luka 4:14-15)
14Baada ya Yahya kutiwa gerezani, Isa alienda Galilaya, akaanza kuhubiri Injili ya Mungu, 15akisema, “Wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Injili.”
Wanafunzi wa kwanza wa Isa
(Mathayo 4:18-22; Luka 5:1-11; Yohana 1:35-51)
16Isa alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa walikuwa wavuvi. 17Isa akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 18Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.
19Alipoenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Isa.
Isa atoa pepo mchafu
(Luka 4:31-37)
21Wakaenda hadi Kapernaumu. Mara ilipofika siku ya Sabato, Isa akaingia sinagogi#1:21 Nyumba ya ibada na mafunzo., akaanza kufundisha. 22Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama walimu wa Torati. 23Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapaza sauti akisema, 24“Tuna nini nawe, Isa Al-Nasiri? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
25Lakini Isa akamkemea, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” 26Yule pepo mchafu akamgaragaza huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.
27Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” 28Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.
Isa amponya mama mkwe wa Simoni na pia watu wengi
(Mathayo 8:14-17; Luka 4:38-41)
29Mara walipotoka katika sinagogi, walienda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani mwa Simoni na Andrea. 30Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Isa habari zake. 31Hivyo Isa akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.
32Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Isa wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34Isa akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.
Isa aenda Galilaya
(Luka 4:42-44)
35Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Isa akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba. 36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta, 37nao walipomwona, wakapaza sauti, wakasema, “Kila mtu anakutafuta!”
38Isa akawajibu, “Twendeni mahali pengine, kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia. Maana nilikuja kwa kusudi hili.” 39Kwa hiyo akazunguka Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.
Isa amtakasa mtu mwenye ukoma
(Mathayo 8:1-4; Luka 5:12-16)
40Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Isa, akapiga magoti, akimwomba, “Ukitaka, unaweza kunitakasa.”
41Isa, akiwa amejawa na huruma, akaunyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.
43Baada ya Isa kumwonya vikali, akamruhusu aende zake mara moja; 44akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” 45Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Isa hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi bali alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Currently Selected:

Marko 1: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in