Hesabu 31
31
Kulipiza Kisasi Juu Ya Wamidiani
1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Uwalipize kisasi Wamidiani kwa ajili ya Waisraeli. Halafu baada ya hayo, utakufa.”
3 Kwa hiyo Mose akawaambia watu, “Waandaeni baadhi ya wanaume wenu waende vitani kupigana na Wamidiani ili wawalipize kisasi cha Bwana. 4Peleka wanaume 1,000 vitani kutoka kila kabila la Israeli.” 5Kwa hiyo waliandaliwa wanaume 12,000 kwa vita, wanaume 1,000 kutoka kila kabila, walitolewa kutoka koo za Israeli. 6 Mose aliwatuma vitani, watu 1,000 kutoka kila kabila, pamoja na Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, ambaye alichukua vyombo vya mahali patakatifu na tarumbeta za kuashiria.
7 Walipigana dhidi ya Wamidiani, kama Bwana alivyomwagiza Mose, nao waliua kila mwanaume. 8 Miongoni mwa watu waliouawa walikuwepo wafalme watano wa Midiani, nao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba. Vilevile walimuua Balaamu mwana wa Beori kwa upanga. 9 Waisraeli waliwateka wanawake wa Kimidiani pamoja na watoto wao na walichukua makundi ya ngʼombe, kondoo na mali zao kama nyara. 10 Walichoma moto miji yote ambayo Wamidiani walikuwa wanaishi, pamoja na kambi zao zote. 11 Walichukua nyara zote na mateka, pamoja na watu na wanyama, 12 nao waliwaleta wafungwa mateka na nyara kwa Mose na kwa kuhani Eleazari, nao Waisraeli walikusanyika kwenye kambi zao katika tambarare za nchi ya Moabu, kando ya Yordani ngʼambo ya Yeriko.
13Mose, kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya wakatoka kuwalaki nje ya kambi. 14 Mose aliwakasirikia maafisa wa jeshi, yaani hao wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, ambao walirudi kutoka vitani.
15 Mose akawauliza, “Je, mmewaacha wanawake wote hai?” 16 “Wanawake hao ndio waliofuata ushauri wa Balaamu, nao ndio waliowasababisha Waisraeli wamwasi Bwana kwa kile kilichotokea kule Peori, na kwa hiyo pigo liliwapata watu wa Bwana. 17 Sasa waue wavulana wote. Pia muue kila mwanamke ambaye alikwisha fanya tendo la ndoa, 18lakini mwacheni hai kwa ajili yenu kila msichana ambaye kamwe hajawahi kuzini na mwanaume.
19 “Ninyi nyote ambao mmeua mtu yeyote au kumgusa mtu yeyote ambaye ameuawa, lazima mkae nje ya kambi kwa muda wa siku saba. Katika siku ya tatu na ya saba lazima mjitakase wenyewe pamoja na wafungwa wenu. 20 Takaseni kila vazi pamoja na kila kitu kilichotengenezwa kwa ngozi, kwa singa za mbuzi au kwa mti.”
21Kisha kuhani Eleazari aliwaambia askari waliokuwa wamekwenda vitani, “Haya ndiyo matakwa ya sheria ambayo Bwana alimpa Mose: 22 Dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati, risasi, 23 na kitu kingine chochote ambacho kinaweza kuhimili moto lazima mkipitishe kwenye moto, kisha kitakuwa safi. Lakini ni lazima pia kitakaswe kwa maji ya utakaso. Kitu chochote kisichoweza kuhimili moto lazima kipitishwe kwenye yale maji ya utakaso. 24 Katika siku ya saba fueni nguo zenu, nanyi mtakuwa safi. Kisha mtaweza kuingia kambini.”
Kugawanya Mateka
25 Bwana akamwambia Mose, 26 “Wewe na kuhani Eleazari pamoja na viongozi wa jamaa ya jumuiya mtahesabu watu wote na wanyama ambao walitekwa. 27 Gawanyeni hizo nyara kati ya askari ambao walishiriki katika vita na kwa jumuiya. 28 Kutoka fungu la wale waliokwenda kupigana vitani, tenga kama ushuru kwa ajili ya Bwana kitu kimoja kati ya kila mia tano, ikiwa ni wanadamu, ngʼombe, punda, kondoo au mbuzi. 29Chukua ushuru huu kutoka fungu lao, umpe kuhani Eleazari kama sehemu ya Bwana. 30 Kutoka fungu la Waisraeli, chukua kitu kimoja kati ya kila hamsini, ikiwa ni wanadamu, ngʼombe, punda, kondoo, mbuzi au wanyama wengine. Hivyo uwape Walawi, ambao wanawajibika kutunza Maskani ya Bwana.” 31Kwa hiyo Mose na kuhani Eleazari wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Mose.
32Nyara zilizobaki kutoka mateka ambayo askari walichukua ni kondoo 675,000, 33ngʼombe 72,000, 34punda 61,000, 35na wanawake 32,000 ambao hawakumjua mume kwa kufanya tendo la ndoa.
36Nusu ya fungu la wale waliokwenda kupigana vitani lilikuwa:
Kondoo 337,500 37 ambayo ushuru kwa ajili ya Bwana ilikuwa kondoo 675;
38ngʼombe 36,000 ambao ushuru kwa ajili ya Bwana ulikuwa ngʼombe 72;
39punda 30,500 ambao ushuru kwa ajili ya Bwana ulikuwa punda 61;
40Watu 16,000 ambao ushuru kwa ajili ya Bwana ulikuwa watu 32.
41 Mose alimpa kuhani Eleazari ushuru kama sehemu ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
42Ile nusu iliyokuwa ya Waisraeli, ambayo Mose aliitenga kutoka kwa ile ya watu waliokwenda vitani, 43nusu iliyokuwa ya jumuiya, ilikuwa kondoo 337,500, 44ngʼombe 36,000, 45punda 30,500, 46na wanadamu 16,000. 47Kutoka hiyo nusu iliyokuwa ya Waisraeli, Mose alichagua moja kati ya kila hamsini ya wanadamu na wanyama, kama Bwana alivyomwagiza, naye aliwapa Walawi, ambao waliwajibika kutunza Maskani ya Bwana.
48Kisha maafisa waliokuwa juu ya vikosi vya jeshi, wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, walimwendea Mose 49 na kumwambia, “Watumishi wako wamehesabu askari walio chini ya amri yetu na hakuna hata mmoja aliyekosekana. 50 Kwa hiyo tumeleta kama sadaka kwa Bwana vyombo vya dhahabu kila mmoja wetu alivyopata, yaani vikuku, bangili, pete za muhuri, vipuli na mikufu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yetu mbele za Bwana.”
51Mose na kuhani Eleazari wakapokea kutoka kwao dhahabu, yaani vyombo vyote vilivyonakshiwa. 52Dhahabu yote kutoka kwa wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia ambavyo Mose na kuhani Eleazari walimletea Bwana kama zawadi ilikuwa shekeli 16,750#31:52 Shekeli 16,750 ni sawa na kilo 200. 53 Kila askari alikuwa amejichukulia nyara zake binafsi. 54 Mose na kuhani Eleazari walipokea dhahabu kutoka kwa wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, wakazileta katika Hema la Kukutania kama ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Bwana.
Currently Selected:
Hesabu 31: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.