YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 144

144
Zaburi 144
Mfalme amshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushindi
Zaburi ya Daudi.
1Ahimidiwe Mwenyezi Mungu Mwamba wangu,
aifundishaye mikono yangu vita,
na vidole vyangu kupigana.
2Yeye ni Mungu wangu wa upendo na ulinzi wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
ngao yangu, ninayemkimbilia,
ambaye huwatiisha mataifa chini yangu.
3Ee Mwenyezi Mungu, mwanadamu ni nini hata umjali,
Binadamu ni nini hata umfikirie?
4Mwanadamu ni kama pumzi,
siku zake ni kama kivuli kinachopita.
5Ee Mwenyezi Mungu, pasua mbingu zako, ushuke,
gusa milima ili itoe moshi.
6Peleka umeme uwatawanye adui,
lenga mishale yako uwashinde.
7Nyoosha mkono wako kutoka juu,
nikomboe na kuniokoa
kutoka maji makuu,
kutoka mikononi mwa wageni
8ambao vinywa vyao vimejaa uongo,
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
9Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia,
10kwa Yule awapaye wafalme ushindi,
ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake,
kutokana na upanga hatari.
11Nikomboe na uniokoe
kutoka mikononi mwa wageni
ambao vinywa vyao vimejaa uongo,
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
12Kisha wana wetu wakati wa ujana wao
watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri,
binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa
kurembesha jumba la kifalme.
13Ghala zetu zitajazwa
aina zote za mahitaji.
Kondoo wetu watazaa kwa maelfu,
kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu;
14maksai wetu watakokota
mizigo mizito.
Hakutakuwa na kubomoka kuta,
hakuna kuchukuliwa mateka,
wala kilio cha taabu
katika barabara zetu.
15Heri watu ambao hili ni kweli;
heri wale ambao Mwenyezi Mungu ni Mungu wao.

Currently Selected:

Zaburi 144: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in