Zaburi 27:1-14
Zaburi 27:1-14 NENO
Mwenyezi Mungu ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Mwenyezi Mungu ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wale nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi linizingire pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri. Jambo moja ninamwomba Mwenyezi Mungu, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Mwenyezi Mungu na kumtafuta hekaluni mwake. Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema lake, na kuniweka juu kwenye mwamba. Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia Mwenyezi Mungu na kumsifu. Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Mwenyezi Mungu, unihurumie na unijibu. Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, Mwenyezi Mungu “Nitautafuta.” Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu. Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, Mwenyezi Mungu atanipokea. Nifundishe njia yako, Ee Mwenyezi Mungu, niongoze katika njia iliyo nyoofu, kwa sababu ya watesi wangu. Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri. Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa Mwenyezi Mungu katika nchi ya walio hai. Mngojee Mwenyezi Mungu; uwe hodari na mwenye moyo mkuu, na umngojee Mwenyezi Mungu.