Zaburi 42
42
KITABU CHA PILI
(Zaburi 42–72)
Zaburi 42
Maombi Ya Mtu Aliye Uhamishoni
Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.
1 Kama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji,
ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku, Ee Mungu.
2 Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai.
Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?
3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu
usiku na mchana,
huku watu wakiniambia mchana kutwa,
“Yuko wapi Mungu wako?”
4 Mambo haya nayakumbuka
ninapoimimina nafsi yangu:
Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu,
nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu,
kwa kelele za shangwe na za shukrani
katikati ya umati uliosherehekea.
5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa sababu bado nitamsifu,
Mwokozi wangu na 6 Mungu wangu.
Nafsi yangu inasononeka ndani yangu;
kwa hiyo nitakukumbuka
kutoka nchi ya Yordani,
katika vilele vya Hermoni,
kutoka Mlima Mizari.
7 Kilindi huita kilindi,
katika ngurumo za maporomoko ya maji yako;
mawimbi yako yote pamoja na viwimbi
vimepita juu yangu.
8 Mchana Bwana huelekeza upendo wake,
usiku wimbo wake uko nami:
maombi kwa Mungu wa uzima wangu.
9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu,
“Kwa nini umenisahau?
Kwa nini niendelee kuomboleza,
nikiwa nimeonewa na adui?”
10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali
adui zangu wanaponidhihaki,
wakiniambia mchana kutwa,
“Yuko wapi Mungu wako?”
11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa sababu bado nitamsifu,
Mwokozi wangu na Mungu wangu.
Currently Selected:
Zaburi 42: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.