Warumi 6
6
Kufa Na Kufufuka Pamoja Na Kristo
1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka? 2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi? 3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? 4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.
5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake. 6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi. 7 Kwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.
8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye. 9 Kwa maana tunajua kwamba Kristo, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake. 10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.
11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. 12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.
Watumwa Wa Haki
15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha! 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.
19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa. 20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki. 21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti. 22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele. 23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Currently Selected:
Warumi 6: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.