Ruthu Utangulizi
Utangulizi
Kitabu hiki kimepewa jina la Ruthu, mhusika mkuu katika habari zilizoandikwa humu. Elimeleki na mkewe Naomi walilazimika kuhama kutoka Bethlehemu kwenda nchi ya Moabu. Muda mfupi baadaye Elimeleki akafariki, nao wanawe Maloni na Kilioni nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, Ruthu na Orpa. Maloni na Kilioni wakafariki bila watoto. Naomi alipoamua kurudi nyumbani kwake katika nchi ya Yuda, aliwashawishi wakwe zake kurudi kwao. Ruthu alisisitiza kwenda pamoja naye, lakini Orpa aliamua kurudi nyumbani kwao.
Naomi na Ruthu walipofika Israeli, Ruthu alienda kutafuta riziki yao. Alijikuta katika mashamba ya mtu wa jamaa wa karibu wa Elimeleki, kwa jina Boazi, ambaye aliamuru Ruthu atunzwe na wafanyi kazi wake. Baada ya muda, Boazi alimwoa Ruthu. Ukoo wa ufalme wa Israeli ulioanza na Mfalme Daudi ulitoka ukoo huu. Baadaye Masiya, Yesu Kristo, anatajwa kuwa wa ukoo huu.
Mwandishi
Hajulikani, lakini mapokeo ya Kiyahudi yanasema Samweli ndiye mwandishi.
Kusudi
Kitabu cha Ruthu kinaonyesha jinsi watu watatu wanaweza kuwa na mwenendo thabiti na wa uadilifu kwa Mungu wakati jamii inayowazunguka imepotoka.
Mahali
Moabu na Bethlehemu.
Tarehe
Baada ya kipindi cha Waamuzi, 1375–1050 K.K.
Wahusika Wakuu
Naomi, Ruthu na Boazi.
Wazo Kuu
Uhusiano kati ya Naomi na mkwewe Ruthu unatupa kielelezo jinsi maisha ya kumcha Mungu yanapasa kuwa, na vile upendo wa kweli kwa jirani unavyoweza kuwa na matokeo ya baraka.
Mambo Muhimu
Kuambatana kwa Ruthu na Naomi kunaonyesha uaminifu wa Ruthu, ijapokuwa Naomi alimsihi arudi kwa watu wake baada ya kufiwa na mumewe. Kutokana na uaminifu huo, Ruthu anatajwa katika uzao wa Yesu kutokana na kuolewa na Boazi.
Mgawanyo
Naomi kuondoka Israeli, na kurudi kwake (1:1-22)
Ruthu anakaribishwa (2:1–3:18)
Boazi na Ruthu (4:1-22).
Currently Selected:
Ruthu Utangulizi: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.