Matendo UTANGULIZI
UTANGULIZI
Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaendeleza masimulizi ya Injili kadiri ya Luka. Kitabu hiki kinaelezea jinsi ile jumuiya ya Kikristo aliyoanzisha Yesu ilivyoongezeka tangu kufufuka kwake. Jamii hiyo iliendelea kukua hata wakati mtume Paulo alipowasili Rumi akitangaza Habari Njema kwa uhodari na bila kizuizi (Mdo 28:31).
Katika kitabu hiki kuna sehemu nne ambazo mwandishi anatumia nafsi ya kwanza wingi yaani (sisi) katika masimulizi yake: 16:10-17; 20:5-15; 21:1-18; 27:1—28:16. Sehemu hizi zote zinahusika na safari baharini na zinaonekana kuwa ni kumbukumbu zilizowekwa na Luka juu ya matukio ya siku kwa siku ya safari zake na msafiri mwenzake Paulo ambaye alikuwa naye kule Filipi, Yerusalemu, Kaisaria, Antiokia (ambamo kwa mara ya kwanza wafuasi wa Yesu wanaitwa “Wakristo”) (Mdo 11:2) na katika safari ya kwenda Rumi.
Shabaha ya Luka ni kumhakikishia Theofilo juu ya ukweli wa “mambo yote Yesu aliyoyatenda na kufundisha” (Mdo 1:1-2; Lk 1:1-4) na jinsi Ukristo ulivyoenea ulimwenguni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu (1:8). Mwandishi anahakiki kuwa Ukristo ni imani adili na kwamba vuguvugu hilo la Ukristo halikuwa la uasi uliotishia dini ya Kiyahudi wala dola la Kirumi. Aidha hakuna hata hakimu mmoja au wakuu wa serikali waliomsikiliza Paulo ambao waliwagundua hao Wakristo kuwa na hatia yoyote ile.
Kwa muhtasari kitabu hiki chaweza pia kuitwa, “Kitabu cha Matendo ya Roho Mtakatifu” maana mada ya kudumu katika habari zake zote ni ile inayoonesha jinsi nguvu ya Roho Mtakatifu ilivyowaimarisha na kuwasukuma wanajumuiya wa kanisa changa. Kitabu cha Matendo ya Mitume chaweza pia kuitwa “Kitabu cha Kwanza cha Historia ya Kanisa”, maana ndivyo kilivyo, hatua kwa hatua.
Kitabu hiki chaweza kugawanywa katika kile tunachoweza kuita “Hatua” tatu kubwa, kulingana na vituo vya kijiografia vinavyohusiana na matukio mbalimbali:
1. Hatua ya kwanza: Yerusalemu (2:1—8:3). Baada ya Yesu kufufuka na kupaa mbinguni (1:4-11) Yerusalemu ndicho kituo cha uumbikaji wa kiini cha kale cha Ukristo (1:12-26). Hapo ndipo Roho Mtakatifu alipowashukia mitume na wafuasi wa Yesu (2:4); hapo ndipo hatua za kwanza za muundo wa kanisa zilipofanyika (2:41—8:3).
2. Hatua ya pili: Yudea na Samaria (8:4—9:43). Tukio la kuwatesa Wakristo lililoanza mara baada ya hotuba ya Stefano (6:9—7:60) liliwafanya wengi wao kuondoka Yerusalemu na “kutawanyika katika nchi ya Yudea na Samaria” (8:1). Tukio hilo lilisadia kuenea kwa Injili ambayo wakati huo ilikuwa imeanza katika sehemu mbalimbali za Siria na Palestina (4:4-6,25-26; 9:19,30-32,35-36,38,42-43).
3. Hatua ya tatu: kuenea kwa Injili mpaka miisho ya dunia (10:1—28:31). Sauli wa Tarso alipokuwa katika kilele cha bidii yake ya kuwatesa Wakristo, alipokuwa anakwenda Dameski, Mungu alimwita ili amfanye kuwa chombo chake cha kuwaaplekea watu wa mataifa mengine Injili (9:15). Vile vile wale waumini waliotawanyika kwa sababu ya mateso yale walienea mpaka Foinike, Kipro na Antiokia (11:19) na kwa njia yao mlango wa kuwafikia watu wengine na Injili ulifunguliwa. Kitabu kina masimulizi juu ya safari tatu za mtume Paulo za kueneza Injili: tangu Asia Ndogo, Europa kwa kupitia Makedonia na kufika Akaya (13:1—14:28; 15:36—18:22; 18:23—20:38). Mwishoni mwa safari yake ya tatu anarudi Yerusalemu (21:1-15) ambapo alikamatwa hekaluni (21:27-30). Sura za mwisho zinaleza mambo yaliyompata Paulo katika safari yake ya kwenda Rumi.
Currently Selected:
Matendo UTANGULIZI: SRUVDC
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.