YouVersion Logo
Search Icon

2 Wakorintho 12

12
Maono na mafunuo ya Paulo
1Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikia maono na mafunuo ya Bwana. 2Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. 3Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); 4#Lk 23:43; Ufu 2:7 ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haistahili mwanadamu ayaseme. 5#2 Kor 11:30 Kuhusu mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa kuhusu udhaifu wangu. 6#2 Kor 10:8; 11:16 Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu. 7#Ayu 2:6 Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nilipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. 8Kwa ajili ya kitu hicho nilimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. 9Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10#Flp 4:13 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na matusi, na matatizo, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Shauku ya Paulo kwa kanisa la Korintho
11 # 2 Kor 11:5 Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lolote, nijapokuwa si kitu. 12#Rum 15:19 Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika subira yote, kwa ishara na maajabu na miujiza. 13#2 Kor 11:19 Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe kosa hili.
14 # 2 Kor 13:1 Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto. 15#Flp 2:17 Nami nitakuwa radhi kutumia na kutumiwa kwa ajili yenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa? 16Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu niliwapata kwa hila. 17Je! Mtu yeyote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo niliwatoza kitu? 18#2 Kor 8:6,16-18 Nilimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile?
19Mnadhani hata sasa ya kuwa najitetea kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi. 20#2 Kor 10:2; 1 Kor 4:6 Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia; 21#2 Kor 2:1; 13:2 nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na uovu walioufanya.

Currently Selected:

2 Wakorintho 12: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in