YouVersion Logo
Search Icon

Matendo 11

11
Ripoti ya Petro kwa kanisa katika Yerusalemu
1Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Yudea wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. 2#Mdo 10:45 Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, 3#Gal 2:12; Efe 2:11 wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. 4Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, 5#Mdo 10:9-48 Nilikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inateremshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. 6Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, wale watambaao, na ndege wa angani. 7Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. 8Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijawahi kuingia kinywani mwangu. 9Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. 10Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. 11Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. 12Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; 13akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, 14atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. 15Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. 16#Mdo 1:5 Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu. 17Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? 18#Mdo 13:48; 14:27 Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.
Kanisa la Antiokia
19 # Mdo 8:1-4 Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. 20Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kigiriki, wakihubiri Habari Njema za Bwana Yesu. 21#Mdo 2:47 Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. 22#Mdo 4:36 Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hadi Antiokia. 23#Mdo 13:43 Naye, alipofika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa moyo wote. 24#Mdo 5:14; 6:5 Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. 25#Mdo 9:30 Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; 26#Gal 2:11; Mdo 26:28; 1 Pet 4:16 hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.
27 # Mdo 13:1; 15:32 Siku zizo hizo manabii waliteremka kutoka Yerusalemu hadi Antiokia. 28#Mdo 21:10 Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. 29#Gal 2:10 Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Yudea. 30#Mdo 12:25 Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

Currently Selected:

Matendo 11: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

Videos for Matendo 11