YouVersion Logo
Search Icon

Waefeso 4

4
Umoja katika mwili wa Kristo
1 # Kol 1:10 Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; 2#Kol 3:12-13 kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; 3#Kol 3:14,15 na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. 4#Rum 12:5 Kuna mwili mmoja, na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
5 # Yn 10:16; 1 Kor 8:6 Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. 6#1 Kor 12:6 Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. 7#Rum 12:3,6; 1 Kor 12:11 Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. 8#Zab 68:18; Kol 2:15 Hivyo husema,
Alipopaa juu aliteka mateka,
Akawapa wanadamu vipawa.
9 # Yn 3:13 Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi? 10Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. 11#1 Kor 12:28; Mdo 21:8 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 12#1 Pet 2:5; 2 Tim 3:17 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 13#Kol 1:28 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 14#1 Kor 14:20; Ebr 13:9 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. 15#Efe 1:22; 5:23; Kol 1:18 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. 16#Kol 2:19 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.
Maisha ya zamani na mapya
17 # Rum 1:21; Kol 2:4,6 Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msiende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; 18#Efe 2:12; Kol 1:21; 1 Pet 1:14 ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wametengwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; 19#Kol 3:5 ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani. 20Bali ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo; 21ikiwa kwa hakika mlisikia habari zake na kufundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, 22#Kol 3:9; Rum 8:13; Gal 6:8 mvue mwenendo wenu wa kwanza, utu wa zamani unaoharibika, kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; 23#Rum 12:2 na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; 24#Mwa 1:26; Kol 3:10 na mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.
Amri za maisha mapya
25 # Zek 8:16; Kol 3:8 Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. 26#Zab 4:4; Yak 1:19,20 Muwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; 27wala msimpe Ibilisi nafasi. 28#1 The 4:11 Mwizi asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akifanya kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. 29#Efe 5:4; Kol 3:16,17; 4:6 Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. 30#Efe 1:13; Isa 63:10 Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa mhuri hata siku ya ukombozi. 31#Kol 1:5 Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matusi yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; 32#Kol 3:13; Mt 6:14; 18:22-35 tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

Currently Selected:

Waefeso 4: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in