YouVersion Logo
Search Icon

Ezekieli 40

40
Maono ya hekalu jipya
1 # Eze 33:21; 1:3 Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, akanileta huko. 2#Eze 8:3; Ufu 21:10 Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini. 3#Dan 10:6; Eze 47:3; Ufu 11:1; 21:15 Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa kupimia; akasimama karibu na lango. 4#Eze 2:7,8; 3:17; 43:10 Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako, ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuoneshe haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli.
5 # Isa 26:1; 1 Fal 6:1-38; 2 Nya 3:1-9 Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja. 6Kisha akaenda hadi katika lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake; akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana wake mwanzi mmoja. 7#1 Nya 9:18 Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. 8Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. 9Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na ukumbi wa lango uliielekea nyumba. 10#1 Nya 26:12,13; Wim 1:4; Neh 13:5,9,12,13; Isa 26:20; Yer 35:2 Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na kipimo kimoja, upande huu na upande huu. 11Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango, dhiraa kumi na tatu. 12Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu. 13Akalipima lango, toka paa la chumba kimoja hadi paa la chumba cha pili, upana wa dhiraa ishirini na tano; mlango mmoja ukielekea mlango wa pili. 14#Kut 27:9; Law 6:16; Zab 85:4; 84:2; 87:4; 100:4; Isa 54:2; 60:8,9; 62:9; Eze 8:7; 42:1 Akafanya miimo pia, dhiraa sitini; na uwanda uliufikia mwimo, lango lile likizungukwa pande zote. 15Na toka mahali palipo mbele ya lango, penye maingilio yake, hata mahali palipo mbele ya ukumbi wa ndani ya lango, dhiraa hamsini. 16Na kwa vile katika vyumba palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na kwa miimo yake ndani ya lango pande zote, na kwa matao yake vivyo hivyo; na madirisha yalikuwako, pande zote upande wa ndani, tena palikuwa na mitende juu ya kila mwimo.
17 # Ufu 11:2; Eze 45:5 Ndipo akanileta mpaka katika ua wa nje, na tazama, palikuwa na vyumba, na sakafu iliyofanyizwa kwa ule ua pande zote; vyumba thelathini vilikuwako juu ya sakafu ile. 18Na ile sakafu ilikuwa kando ya malango, urefu wake sawasawa na urefu wa malango, yaani, sakafu ya chini. 19Kisha akaupima upana, toka mahali palipokuwa mbele ya lango la chini hadi mahali palipokuwa mbele ya ua wa ndani, nje yake, dhiraa mia moja upande wa mashariki, na upande wa kaskazini. 20Nalo lango la ua wa nje, lililoelekea kaskazini, akalipima urefu wake, na upana wake. 21Na vyumba vyake vya walinzi vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; na miimo yake, na matao yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango la kwanza; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. 22Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na matao yake yalikuwa mbele yake. 23Na ule ua wa ndani ulikuwa na lango lililoelekea lile lango la pili, upande wa kaskazini, na upande wa mashariki; akapima toka lango hadi lango, dhiraa mia moja. 24Akanileta mpaka upande wa kusini, na tazama, lango lililoelekea kusini; akaipima miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo. 25#1 Fal 6:4; Isa 54:12 Tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote kama madirisha hayo; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. 26Tena palikuwa na madaraja saba ya kulipandia, na matao yake yalikuwa mbele yake; nalo lilikuwa na mitende, mmoja upande huu, na mmoja upande huu, juu ya miimo yake. 27Tena ua wa ndani ulikuwa na lango, lililoelekea kusini; akapima toka lango hadi lango, kwa kuelekea upande wa kusini, dhiraa mia moja.
28Kisha akanileta mpaka ua wa ndani karibu na lango lililoelekea kusini; akalipima lango la kusini kwa vipimo vivyo hivyo; 29#1 Fal 6:5-10; 1 Nya 28:11,12; 2 Nya 3:9; 31:11; Neh 10:38,39; 12:44; 13:5,9,12,13; Yer 35:2; 36:10 navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. 30Tena palikuwa na matao pande zote, urefu wake dhiraa ishirini na tano na upana wake dhiraa tano. 31#Zab 92:12; Wim 7:7; Yer 10:5 Na matao yake yaliuelekea ua wa nje, na mitende ilikuwa juu ya miimo yake; palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. 32Akanileta mpaka ua wa ndani ulioelekea upande wa mashariki, akalipima lango kwa vipimo vivyo hivyo; 33navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, kwa vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. 34Na matao yake yaliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. 35Akanileta mpaka lango lililoelekea upande wa kaskazini; akalipima kwa vipimo vivyo hivyo; 36vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake; tena palikuwa na madirisha ndani yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. 37Na miimo yake iliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
38 # Law 1:9; 3:11; Ebr 9:14 Na chumba, pamoja na lango lake, kilikuwa karibu na miimo ya malango; ndiko walikoiosha sadaka ya kuteketezwa. 39#Law 4:2,3; 5:6; 6:6; 7:1; 14:12,13; 19:21,22; Isa 53:5; 2 Kor 5:21; Tit 2:14; Ebr 10:12-14; 1 Pet 1:18,19; Ufu 5:9; Hes 6:12; Eze 42:13; 44:29 Na katika ukumbi wa lango palikuwa na meza mbili upande huu, na meza mbili upande huu, ili kuichinja sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia. 40Na upande mmoja, nje, penye madaraja ya kuliingia lango lililoelekea kaskazini, palikuwa na meza mbili; na upande wa pili, ulio wa ukumbi wa lango hilo, palikuwa na meza mbili. 41Palikuwa na meza nne upande huu, na meza nne upande huu, karibu na lango; meza nane ambazo juu yake walizichinja sadaka. 42Tena palikuwa na meza nne kwa sadaka za kuteketezwa, za mawe yaliyochongwa; urefu wake dhiraa moja na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja; juu yake waliviweka vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka. 43Tena hizo kulabu, ambazo urefu wake ni shubiri, zilifungwa ndani pande zote; na juu ya meza hizo ilikuwako nyama ya matoleo. 44#1 Nya 6:31; Kol 3:16; Efe 5:19 Tena nje ya lango la ndani palikuwa na vyumba kwa waimbaji, katika ua wa ndani, uliokuwa kando ya lango lililoelekea kaskazini, navyo vilikabili upande wa kusini; na kimoja kando ya lango lililoelekea upande wa mashariki, kilikabili upande wa kaskazini. 45#Law 8:35; Hes 3:7; Kum 11:1; 1 Fal 2:3; Ufu 1:6 Akaniambia, Chumba hiki kinachokabili upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani, yaani, hao wasimamizi wa nyumba. 46#Hes 18:5; 1 Fal 2:35; Eze 44:15; 43:19; Efe 2:17; Kol 4:12 Nacho chumba kinachokabili upande wa kaskazini ni cha makuhani, wasimamizi wa madhabahu; hao ni wana wa Sadoki, ambao kati ya wana wa Lawi, ndio waliomkaribia BWANA, ili kumtumikia. 47Akaupima huo ua, na urefu wake ulikuwa dhiraa mia moja, na upana wake dhiraa mia moja, mraba; nayo madhabahu yalikuwa mbele ya nyumba.
Hekalu
48Ndipo akanileta mpaka ukumbi wa nyumba, akapima kila mwimo wa ukumbi, dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; na upana wa lango ulikuwa dhiraa tatu upande huu, na dhiraa tatu upande huu. 49#1 Fal 6:3; 7:21 Urefu wa ukumbi ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi na moja; karibu na madaraja ambayo waliupandia; tena palikuwa na nguzo karibu na miimo, moja upande huu, na moja upande huu.

Currently Selected:

Ezekieli 40: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

Videos for Ezekieli 40