YouVersion Logo
Search Icon

Waraka kwa Waebrania 7

7
Utaratibu wa ukuhani wa Melkizedeki
1 # Mwa 14:17-20 Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Abrahamu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; 2ambaye Abrahamu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; 3#Zab 110:4 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.
4Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. 5#Hes 18:21 Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika uzao wa Abrahamu. 6Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Abrahamu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. 7Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. 8Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yuko hai. 9Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Abrahamu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; 10kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye.
Kuhani mwingine kama Melkizedeki
11Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine awepo, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni? 12Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. 13Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hilo aliyeihudumia madhabahu. 14#Mwa 49:10; Isa 11:1 Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambalo Musa hakunena neno lolote juu yake katika mambo ya ukuhani. 15Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine kama Melkizedeki; 16asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na kikomo; 17#Zab 110:4; Ebr 5:6 maana ameshuhudiwa kwamba,
Wewe u kuhani milele
Kwa mfano wa Melkizedeki.
18Maana, kuna kubatiliwa kwa ile amri iliyotangulia, kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake; 19#Ebr 9:9 (kwa maana ile sheria haikukamilisha neno); na pamoja na hayo kuliingizwa matumaini yaliyo mazuri zaidi, ambayo kwa hayo tunamkaribia Mungu. 20Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo, 21#Zab 110:4 (maana wale walifanywa makuhani pasipo kiapo; bali yeye, pamoja na kiapo, kwa yeye aliyemwambia,
Bwana ameapa wala hataghairi,
Wewe u kuhani milele;)
22 # Ebr 8:6; 12:24 basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. 23Tena wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu walizuiliwa na mauti wasikae; 24bali yeye, kwa kuwa anakaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. 25#Rum 8:34; 1 Yoh 2:1 Naye, kwa sababu hii, anaweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.
26 # Ebr 4:14 Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; 27#Law 9:7; 16:6,15 ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. 28#Ebr 5:1,2 Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele.

Currently Selected:

Waraka kwa Waebrania 7: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

Videos for Waraka kwa Waebrania 7