YouVersion Logo
Search Icon

Wafilipi UTANGULIZI

UTANGULIZI
Mji wa Filipi ulikuwa maarufu sana mkoani Makedonia. Ulipewa jina hili kwa heshima ya mfalme Filipo wa Makedonia, babake Iskanda Mkuu (356 Kabla ya Kristo Kuzaliwa).
Paulo, katika safari yake ya pili ya kitume, alihubiri Injili mjini humo. Paulo na Sila walipata kufungwa humo, lakini nguvu ya Mungu ikawatoa gerezani hata mlinzi wa gereza akabatizwa pamoja na jamaa yake yote (Mdo 16:12-40). Kanisa la Filipi lilikuwa la kwanza katika sehemu ya Ulaya. Baadaye Paulo alifanya ziara mbili mjini humo (Mdo 20:1-6; 2 Kor 2:13). Waumini wa Filipi walimpenda Paulo sana, wakampa misaada mbalimbali kwa ajili ya kazi yake (1:7-8; 4:14-17; 2 Kor 11:9).
Waumini wa Filipi walipopata habari za kufungwa kwa Paulo kule Rumi walichanga fedha na vitu mbalimbali wakamtuma Epafrodito aende Rumi ampe msaada huo na kumpasha habari za kanisa la Filipi (4:8). Wasiwasi uliwashika walipopata habari za kuugua kwa Epafrodito akiwa Rumi. Lakini baadaye alipona (2:25-27).
Paulo aliwaandikia Wafilipi waraka huu akiwa kifungoni (1:7,12-17 tazama utangulizi Waraka kwa Waefeso). Baada ya maneno ya shukrani kwa Mungu kama ilivyo kawaida katika nyaraka nyingi (1:3-11), mambo mawili yanajitokeza katika waraka huu: La kwanza ni furaha ambayo inatokana na imani iliyokomaa, na la pili ni upendo wa Paulo kwa kanisa la Filipi. Haya mawili ni funzo bora la tumaini ambalo mwandishi analirudia tena na tena katika magumu aliyoyapata kifungoni mwake. Katika 1:12-26 Paulo anatamka kwamba hali ya kuwa kifungoni imempa fursa ya kutangaza Injili (1:12-14). Kisha anawaza juu ya huduma yake ya kitume ambayo ataendelea kujitolea kuitekeleza “kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu” (1:20) mradi haujafika wakati atakapokwenda zake akae na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi (1:23) maana kwake Paulo “kuishi ni Kristo na kufa ni faida” (1:21).
Katika 1:27—2:18 kuna azimio rasmi la kimsingi la imani ya Kikristo: utenzi (2:5-11) ambao umetungwa kwa heshima ya Mwana wa Mungu aliyekuwako kabla na aliye milele, yaani Kristo Yesu ambaye “yeye mwanzo alikuwa na namna ya Mungu… alijinyenyekeza… hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” Kwa utii wake “Mungu alimwadhimisha mno” apate kutambuliwa na kuabudiwa kila mahali kama Bwana.
Katika 3:1—4:1 Paulo anataja kwamba huko Filipo kulikuwa na watu ambao ni “maadui wa msalaba wa Kristo” (3:18). Inaonekana pia kwamba watu wengine walifika Filipi ambao walisisitiza kufuata Torati ya Musa na hasa desturi ya kutahiri na hivyo kuwasumbua wale Wakristo wasio Wayahudi.
Katika 4:2-9 Paulo anasisitiza kuwa furaha ya wokovu ni jambo la kudumu katika maisha ya Kikristo (4:4).

Currently Selected:

Wafilipi UTANGULIZI: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in