Luka 23
23
Gavana Pilato Amhoji Yesu
(Mt 27:1-2,11-14; Mk 15:1-5; Yh 18:28-38)
1Kisha kundi lote likasimama, wakampeleka Yesu kwa Pilato. 2Wakaanza kumshitaki Yesu na kumwambia Pilato, “Tumemkamata mtu huyu akijaribu kuwapotosha watu wetu. Anasema tusilipe kodi kwa Kaisari. Anajiita Masihi, mfalme.”
3Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Ndiyo, unaweza kusema hivyo.”
4Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na watu, “Sioni kosa lolote kwa mtu huyu.”
5Lakini waliendelea kusema, “Mafundisho yake yanasababisha matatizo katika Uyahudi yote. Alianzia Galilaya na sasa yupo hapa!”
Pilato Ampeleka Yesu Kwa Herode
6Pilato aliposikia hili, akauliza, “Mtu huyu anatoka Galilaya?” 7Akatambua kuwa Yesu yuko chini ya mamlaka ya Herode. Siku hizo Herode alikuwa Yerusalemu, hivyo Pilato alimpeleka Yesu kwake.
8Herode alipomwona Yesu alifurahi sana. Alikuwa akisikia habari zake na kwa muda mrefu alikuwa anataka kukutana na Yesu. Herode alitaka kuona muujiza, hivyo alitegemea kwamba Yesu angefanya muujiza mmoja. 9Akamwuliza Yesu maswali mengi, lakini Yesu hakusema chochote. 10Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wamesimama pale wakipaza sauti zao wakimshitaki kwa Herode. 11Ndipo Herode na askari wake wakamcheka. Wakamfanyia mzaha kwa kumvalisha mavazi kama ambayo wafalme huvaa. Kisha Herode akamrudisha Yesu kwa Pilato. 12Nyakati za nyuma Pilato na Herode walikuwa maadui daima. Kuanzia siku ile wakawa marafiki.
Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu
(Mt 27:15-26; Mk 15:6-15; Yh 18:39–19:16)
13Pilato aliwaita viongozi wa makuhani, viongozi wa Kiyahudi na watu wote pamoja. 14Akawaambia, “Mlimleta mtu huyu kwangu. Mlisema alikuwa anawapotosha watu. Lakini nimemchunguza mbele yenu nyote na sijaona hatia juu ya kitu chochote mnachomshitakia. 15Hata Herode hakumwona kuwa ana hatia yoyote. Akamrudisha kwetu. Tazameni, hajafanya jambo lolote baya linalostahili adhabu ya kifo. 16Kwa hiyo, baada ya kumwadhibu kidogo nitamwacha aende zake.” 17#23:17 Nakala chache za Kiyunani zimeongeza mstari wa 17: “Kila mwaka wakati wa Siku Kuu ya Pasaka, ilimpasa Pilato kumwachia huru mfungwa mmoja.”
18Lakini wote walipaza sauti zao pamoja, “Mwue! Mwachie huru Baraba!” 19(Baraba alifungwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo mjini na kwa mauaji.)
20Pilato alitaka amwachie huru Yesu. Hivyo Pilato akawaambia atamwachilia. 21Lakini walipaza sauti tena wakisema, “Mwue, Mwue msalabani!”
22Mara ya tatu Pilato akawaambia watu, “Kwa nini? Amefanya kosa gani? Hana hatia. Sioni sababu ya kumwua. Hivyo nitamwachia huru baada ya kumwadhibu kidogo.”
23Lakini watu waliendelea kupaza sauti. Walidai Yesu auawe msalabani. Kelele zao zikawa kubwa kiasi kwamba 24Pilato aliamua kuwapa kile walichotaka. 25Walitaka Baraba aliyekuwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo na mauaji aachiwe huru. Pilato akamwachia Baraba. Na kumtoa Yesu ili auawe. Hili ndilo watu walitaka.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mt 27:32-44; Mk 15:21-32; Yh 19:17-27)
26Askari wakamwongoza Yesu kumtoa nje ya mji. Wakati huo huo mtu mmoja kutoka Kirene alikuwa anaingia mjini kutoka maeneo nje ya Yerusalemu. Askari wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu na kumfuata Yesu kwa nyuma.
27Kundi kubwa wakamfuata Yesu. Baadhi ya wanawake waliokuwemo kwenye kundi walilia na kuomboleza. Walimwonea huruma. 28Lakini Yesu aligeuka na kuwaambia, “Wanawake wa Yerusalemu, msinililie. Jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29Wakati unakuja ambapo watu watasema, ‘Wanawake wasioweza kuwa na watoto ndio ambao Mungu amewabariki. Hakika ni baraka kwamba hawana watoto wa kutunza.’ 30Watu wataiambia milima, ‘Tuangukieni!’ Wataviambia vilima, ‘Tufunikeni!’#Hos 10:8 31Kama hili linaweza kutokea kwa mtu aliye mwema, nini kitatokea kwa wenye hatia?”
32Walikuwepo pia wahalifu wawili waliotolewa nje ya mji pamoja na Yesu ili wauawe. 33Walipelekwa mahali palipoitwa “Fuvu la Kichwa.” Askari walimpigilia Yesu msalabani pale. Waliwapigilia misalabani wahalifu pia, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine kushoto kwa Yesu.
34Na Yesu alikuwa anasema, “Baba uwasamehe watu hawa, kwa sababu hawajui wanalofanya.”
Askari waligawana nguo zake kwa kutumia kamari. 35Watu walisimama pale wakiangalia kila kitu kilichokuwa kinatokea. Viongozi wa Kiyahudi walimcheka Yesu. Walisema, “Kama kweli yeye ni Masihi, Mfalme Mteule wa Mungu, basi ajiokoe. Je! hakuwaokoa wengine?”
36Hata askari walimcheka Yesu na kumfanyia mizaha. Walikuja na kumpa siki ya mvinyo. 37Wakasema, “Ikiwa wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe!” 38Waliandika maneno haya kwenye kibao msalabani juu ya kichwa chake: “Huyu ni Mfalme wa Wayahudi”.
39Mmoja wa wahalifu aliyekuwa ananing'inia pale akaanza kumtukana Yesu: “Wewe siye Masihi? Basi jiokoe na utuokoe sisi pia!”
40Lakini mhalifu mwingine alimnyamazisha asiendelee kumtukana Yesu. Akasema, “Unapaswa kumwogopa Mungu. Sisi sote tutakufa muda si mrefu. 41Wewe na mimi tuna hatia, tunastahili kufa kwa sababu tulitenda mabaya. Lakini mtu huyu hajafanya chochote kibaya.” 42Kisha akamwambia Yesu, “Unikumbuke utakapoanza kutawala kama mfalme!”
43Yesu akamwambia, “Ninakwambia kwa uhakika, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Mk 15:33-41; Yh 19:28-30)
44Ilikuwa yapata saa sita mchana, lakini kulibadilika kukawa giza mpaka saa tisa alasiri, 45kwa sababu jua liliacha kung'aa. Pazia ndani ya Hekalu lilichanika vipande viwili. 46Yesu alipaza sauti akasema, “Baba, ninaiweka roho yangu mikononi mwako!”#Zab 31:5 Baada ya Yesu kusema haya, akafa.
47Mkuu wa askari wa Kirumi aliyekuwa pale alipoona yaliyotokea, alimsifu Mungu, akisema, “Ninajua mtu huyu alikuwa mtu mwema!”
48Watu wengi walikuwa wametoka mjini kuja kuona tukio hili. Walipoona, wakahuzunika, wakaondoka wakiwa wanapiga vifua vyao. 49Watu waliokuwa rafiki wa karibu wa Yesu walikuwepo pale. Pia, walikuwepo baadhi ya wanawake waliomfuata Yesu kutoka Galilaya. Walisimama mbali kutoka msalabani, waliyaona mambo haya.
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Yh 19:38-42)
50-51Mtu mmoja aliyeitwa Yusufu kutoka mji wa Uyahudi ulioitwa Arimathaya alikuwapo pale. Alikuwa mtu mwema, aliyeishi namna Mungu alivyotaka. Alikuwa anausubiri ufalme wa Mungu uje. Yusufu alikuwa mjumbe wa baraza la Kiyahudi. Lakini hakukubali pale viongozi wengine wa Kiyahudi walipoamua kumwua Yesu. 52Alikwenda kwa Pilato na kumwomba mwili wa Yesu. 53Aliushusha mwili kutoka msalabani na kuufunga kwenye nguo. Kisha akauweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika ukuta wa mwamba. Kaburi hili lilikuwa halijatumika bado. 54Ilikuwa jioni Siku ya Maandalizi ya Sabato. Sabato ilikuwa ianze baada ya jua kuzama.
55Wanawake waliotoka Galilaya pamoja na Yesu walimfuata Yusufu. Wakaliona kaburi. Ndani yake wakaona mahali alipouweka mwili wa Yesu. 56Kisha wakaenda kuandaa manukato yanayonukia vizuri ili kuupaka mwili wa Yesu.
Siku ya Sabato walipumzika, kama ilivyoamriwa katika Sheria ya Musa.
Currently Selected:
Luka 23: TKU
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International