Mathayo 14
14
Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji
(Mk 6:14-29; Lk 9:7-9)
1Katika wakati huo, Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia ambacho watu walikuwa wanasema kuhusu Yesu. 2Hivyo akawaambia watumishi wake, “Nadhani hakika mtu huyu ni Yohana Mbatizaji. Lazima amefufuka kutoka kwenye kifo, na ndiyo sababu anaweza kutenda miujiza hii.”
Kifo cha Yohana Mbatizaji
3Kabla ya wakati huu, Herode alimkamata Yohana. Akamfunga kwa minyororo na kumweka gerezani. Alimkamata Yohana kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, kaka yake Herode. 4Yohana alikuwa amemwambia, “Si sahihi kwako kumwoa Herodia.” 5Herode alitaka kumwua, lakini aliwaogopa watu. Waliamini kuwa Yohana alikuwa nabii.
6Siku ya kuzaliwa Herode, bintiye Herodia#14:6 Herodia Josephus, Mwana historia wa Kiyahudi anamwita binti huyu Salome. alicheza mbele yake na kundi lake. Herode alifurahishwa naye sana. 7Hivyo aliapa kuwa atampa kitu chochote atakachotaka. 8Herodia alimshawishi binti yake kitu cha kuomba. Hivyo bintiye akamwambia Herode, “Nipe hapa kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sahani kubwa.”
9Mfalme Herode alihuzunika sana. Lakini alikuwa ameahidi kumpa binti kitu chochote alichotaka. Na watu waliokuwa wakila pamoja na Herode walikuwa wamesikia ahadi yake. Hivyo Herode aliamuru kitu ambacho alikuwa ameomba apatiwe. 10Akawatuma wanaume gerezani, ambako walikikata kichwa cha Yohana. 11Na watu wakakileta kichwa cha Yohana kwenye sahani kubwa na kumpa yule msichana. Kisha yeye akakipeleka kichwa kwa mama yake, Herodia. 12Wafuasi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wa Yohana na kuuzika. Kisha wakaenda na kumwambia Yesu kilichotokea.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mk 6:30-44; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)
13Yesu aliposikia kilichotokea kwa Yohana, aliondoka kwa kutumia mtumbwi. Alikwenda peke yake mpaka mahali ambapo hakuna aliyekuwa akiishi. Lakini watu walisikia kuwa Yesu alikuwa ameondoka. Hivyo waliondoka katika miji na kumfuata. Walikwenda mahali alikokwenda kupitia nchi kavu. 14Yesu alipotoka katika mtumbwi, aliwaona watu wengi. Akawahurumia, na kuwaponya waliokuwa wagonjwa.
15Baadaye mchana huo, wafuasi walimwendea Yesu na kusema, “Hakuna anayeishi katika eneo hili. Na tayari muda umepita, hivyo waage watu ili waende katika miji na kujinunulia chakula.”
16Yesu akasema, “Watu hawahitaji kuondoka. Wapeni ninyi chakula wale.”
17Wafuasi wakajibu, “Lakini tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”
18Yesu akasema, “Leteni kwangu mikate na samaki.” 19Kisha akawaambia watu waketi chini kwenye nyasi. Akaichukua mikate mitano na samaki wawili. Akatazama mbinguni na akamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Kisha akaivunja mikate katika vipande, akawapa wafuasi wake nao wakawapa watu chakula. 20Kila mmoja alikula mpaka akashiba. Walipomaliza kula, wafuasi walijaza vikapu kumi na mbili vya vipande vilivyosalia. 21Walikuwepo wanaume 5,000, pamoja na wanawake na watoto waliokula.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mk 6:45-52; Yh 6:16-21)
22Mara baada ya hili Yesu akawaambia wafuasi wake wapande kwenye mtumbwi. Akawaambia waende upande mwingine wa ziwa. Aliwaambia angekuja baadaye, alikaa pale ili kuwaaga watu. 23Baada ya Yesu kuwaaga watu, alikwenda kwenye vilima peke yake kuomba. Ikawa jioni na alikuwa pale peke yake. 24Wakati huu mtumbwi ilikuwa mbali kutoka pwani. Kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kinyume na mtumbwi, mtumbwi ulikuwa unapata msukosuko kwa sababu ya mawimbi.
25Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, wafuasi wa Yesu walikuwa bado ndani ya mtumbwi. Yesu akaenda kwao akitembea juu ya maji. 26Iliwatisha walipomwona anatembea juu ya maji. Wakapiga kelele kwa woga “Ni mzuka!”
27Lakini haraka Yesu akawaambia, “Msihofu! Ni mimi! Msiogope.”
28Petro akasema, “Bwana, ikiwa hakika ni wewe, niambie nije kwako juu ya maji.”
29Yesu akasema, “Njoo, Petro.”
Kisha Petro akauacha mtumbwi na kutembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30Lakini Petro alipokuwa anatembea juu ya maji, aliyaona mawimbi na upepo. Aliogopa na kuanza kuzama katika maji. Akapiga kelele, “Bwana, niokoe!”
31Haraka Yesu akamshika Petro kwa mkono wake. Akasema, “Imani yako ni ndogo. Kwa nini ulisita?”
32Baada ya Petro na Yesu kuingia kwenye mtumbwi, upepo ukakoma. 33Kisha wafuasi wakamwabudu Yesu na kusema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.”
Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa
(Mk 6:53-56)
34Baada ya kuvuka ziwa, wakafika pwani katika eneo la Genesareti. 35Baadhi ya watu pale wakamwona Yesu na wakamtambua kuwa ni nani. Hivyo wakatuma ujumbe kwa watu wengine katika eneo lote kuwa Yesu amekuja. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote kwake. 36Walimsihi Yesu awaruhusu waguse tu upindo wa vazi lake ili waponywe. Na wagonjwa wote waliogusa vazi lake waliponywa.
Currently Selected:
Mathayo 14: TKU
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International