YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo 22

22
Simulizi Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Sherehe
(Lk 14:15-24)
1Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, 2“Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. 3Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme.
4Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’
5Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. 6Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. 7Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao.
8Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. 9Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ 10Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi.
11Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. 12Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. 13Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’
14Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.”
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mk 12:13-17; Lk 20:20-26)
15Kisha Mafarisayo wakaondoka mahali ambapo Yesu alikuwa anafundisha. Wakapanga mpango wa kumfanya aseme kitu ambacho wangekitumia dhidi yake. 16Wakawatuma kwake baadhi ya wafuasi wao na baadhi ya watu kutoka katika kundi la Maherode. Watu hawa walipofika kwa Yesu wakasema, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu mwema na kwamba daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu, bila kujali ni nani anakusikiliza. Huna wasiwasi namna ambavyo wengine wanaweza wakasema. 17Sasa tuambie, unadhani ni sahihi kulipa kodi kwa Kaisari au la?”
18Lakini Yesu alijua kuwa watu hawa walikuwa wanamtega. Hivyo akasema, “Enyi wanafiki! Kwa nini mnajaribu kunitega ili niseme jambo lililo kinyume? 19Nionesheni sarafu inayotumika kulipa kodi.” Wakamwonesha Yesu sarafu iliyotengenezwa kwa fedha. 20Kisha Yesu akauliza, “Picha iliyo kwenye sarafu hii ni ya nani? Na jina lililo kwenye sarafu hii ni la nani?”
21Wakajibu, “Ni picha ya Kaisari na ni jina la Kaisari.”
Ndipo Yesu akawajibu, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake na mpeni Mungu vilivyo vyake.”
22Waliposikia yale Yesu aliyosema, wakashangaa na kuondoka.
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mk 12:18-27; Lk 20:27-40)
23Siku hiyo hiyo baadhi ya Masadukayo walimjia Yesu. (Masadukayo hawaamini kuwepo kwa ufufuo wa wafu.) Masadukayo walimwuliza Yesu swali. 24Wakasema, “Mwalimu, Musa alituambia kuwa ikiwa mwanaume aliyeoa atakufa na hana watoto, ndugu yake lazima amwoe mkewe ili aweze kuzaa watoto kwa ajili ya nduguye aliyekufa.#22:24 nduguye aliyekufa Tazama Kum 25:5,6. 25Walikuwepo ndugu saba miongoni mwetu. Ndugu wa kwanza alioa lakini akafa bila ya kupata watoto. Hivyo ndugu yake akamwoa mkewe. 26Na ndugu wa pili akafa pia, jambo hili hilo likatokea kwa ndugu wa tatu na ndugu wengine wote. 27Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 28Lakini wanaume wote saba walikuwa wamemwoa. Sasa watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, mwanamke huyu atakuwa mke wa yupi?”
29Yesu akajibu, “Mnakosea sana! Hamjui kile ambacho Maandiko yanasema. Na hamjui lolote kuhusu nguvu ya Mungu. 30Watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawataoa wake na wanawake hawataozwa kwa wanaume. Kila mtu atakuwa kama malaika walio mbinguni. 31Someni kile ambacho Mungu alikisema kuhusu watu kufufuliwa kutoka kwa wafu. 32Mungu alisema, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo.’#Kut 3:6 Ni Mungu wa walio hai tu, hivyo hakika watu hawa hawakuwa wafu.”
33Watu waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho ya Yesu.
Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?
(Mk 12:28-34; Lk 10:25-28)
34Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. 35Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. 36Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?”
37Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’#Kum 6:5 38Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. 39Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako#22:39 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji. kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’#Law 19:18 40Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.”
Je! Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mk 12:35-37; Lk 20:41-44)
41Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je! ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.”
43Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema,
44‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’#22:44 chini ya udhibiti wako Kwa maana ya kawaida, “kuweka chini ya miguu”. #Zab 110:1
45Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?”
46Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi.

Currently Selected:

Mathayo 22: TKU

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in